‘’LIPENI MADENI MNAYODAIWA NA TEMESA, ILI IWEZE KUTEKELEZA WAJIBU WAKE,’’ WAZIRI MKUU MAJALIWA

News Image

Posted On: August 21, 2024

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amezitaka Taasisi zote zinazodaiwa na Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kulipa madeni yao kwa haraka ili kuiwezesha kujiendesha kibiashara na kutoa huduma stahiki kwa wateja wao.

Majaliwa ameyasema hayo Agosti 20 wakati akifungua kongamano la tatu la madereva wa Serikali katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa AICC jijini Arusha ambapo amewataka TEMESA kuandika barua ofisini kwake kuainisha Taasisi zote zinazodaiwa ili kuandikiwa barua ya amri ya kuwalipa.

“Kuna wakati tulifikiria kuifuta TEMESA kwa kulegalega lakini tukawapa muda ila kwa sasa mnafanya kazi vizuri, leteni barua haraka tuwasimamie Taasisi mnazowadai walipe madeni maana hivi sasa hela wanazo kutokana na kuingiziwa katika mwaka huu wa fedha,” amesema Waziri Mkuu.

“Wakuu wa taasisi popote walipo wananisikia, wapo humu ndani, wako nje kupitia vyombo vya Habari walipe madeni yao TEMESA, ili TEMESA yetu itekeleze wajibu wa kuhakikisha vyombo vya usafiri vinakuwa salama na vinatengenezwa kwa wakati”, alisisitiza Waziri Mkuu.

Aidha, Waziri Mkuu ameupongeza Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), kwa kuwa na mitambo ya kisasa ya kutengeneza magari na kuwataka kuongeza ubunifu na uadilifu ili kuleta tija katika utengenezaji wa magari ya Serikali

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi TEMESA Bi Josephine matiro ameishukuru Serikali kwa jitihada zinazofanywa na Wizara ya Ujenzi kwa kuboresha huduma za karakana pamoja na ununuzi wa vifaa vya kisasa na kumuomba Waziri Mkuu kuwashurutisha wakuu wa Taasisi kulipa madeni yao ili kusaidia TEMESA kufanya kazi kiufanisi.