KAMATI YA BUNGE YA MIUNDOMBINU YAISHAURI SERIKALI KUKAMILISHA MIRADI YA UJENZI WA VIVUKO KWA WAKATI
Posted On: March 14, 2025
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeishauri Serikali ihakikishe vivuko vinakarabatiwa na vinakamilika kwa wakati ili wananchi waondokane na adha ya usafiri na usafirishaji katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo eneo la Pangani mkoani Tanga.
Akizungumza leo Wilayani Pangani mara baada ya kukagua mradi wa utekelezaji wa ukarabati wa kivuko cha MV. PANGANI Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Selemani Kakoso amesema kuwa kama siyo ujenzi wa daraja la Pangani wananchi wangepata shida kubwa sana ya usafiri hivyo amesisitiza umuhimu wa Serikali kukarabati kivuko hicho.
“Ujenzi wa daraja umeleta nafuu hivyo hakikisheni mnawawezesha TEMESA kukarabati kivuko hiki ili wananchi wa Pangani wavuke kwa urahisi na salama", amesisitiza Kakoso.
Aidha, Mheshimiwa Kakoso amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa ambao ameuweka kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuwataka wananchi kuiendeleza na kuitunza miradi hiyo ili ilete tija kwa wananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Awali, akiwasilisha taarifa Utekelezaji wa mradihuo Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na umeme Tanzania TEMESA Lazaro Kilahala, amesema kwa mwaka wa fedha 2024/25 Wizara kupitia TEMESAinatekeleza mradi wa ukarabati wa kivuko cha MV. Pangani kitakachotoa huduma kati ya Pangani na Bweni wilayani Pangani ambapo mradi huo unagharimu shilingi bilioni 2.3.