KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MIUNDOMBINU YAITAKA WIZARA KUTATUA CHANGAMOTO ZA TEMESA
Posted On: March 18, 2025
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Selemani Kakoso ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi kuhakikisha fedha ambazo Bunge liliziidhinisha kwa ajili ya matumizi ya Bajeti ikiwemo ujenzi na ukarabati wa vivuko vya Wakala ziweze kuonekana kwa ajili ya kutatua changamoto zinazoikabili TEMESA.
Mhe. Kakoso ameyasema hayo leo wakati kamati hiyo ikiwa na wajumbe wake ilipotembelea kujionea maendeleo ya mradi wa ujenzi wa maegesho ya miundombinu ya Kivuko cha Magogoni-Kigamboni, eneo la kisambusa, Kigamboni jijini Dar es. Salaam.
Akitoa majumuisho baada ya kupokea taarifa za miradi hiyo iliyowasilishwa na Mtendaji Mkuu wa TEMESA Lazaro Kilahala mbele ya Kamati hiyo ya kudumu ya Bunge ya miundombinu, Mhe. Kakoso amesema TEMESA wana miradi ambayo imesimama kwa kukosa fedha za kutekeleza miradi hiyo.
“Tumefanya ukaguzi wa mradi wa kivuko kule Pangani, ule mradi haujapewa fedha zozote, tumefanya ukaguzi leo kwenye eneo la upande wa Kigamboni panaitwa ‘Kisambusa’ na kweli pamekuwa sambusa kabisa kwasababu hamna fedha, Mhe. Naibu Waziri, eneo lile ni muhimu sana, linaleta msongamano wa barabara kwasababu ya miundombinu duni iliyopo pale, kwahiyo tunaomba Mhe. Naibu Waziri sambamba na ule mradi wa kivuko kile kilichoenda kukarabatiwa Mombasa, mkisimamie kiweze kukamilika kwa wakati ili kije kutoa huduma kwa wananchi.” Amesema Mhe. Kakoso huku akiongeza kuwa Wizara ikikamilisha miradi hiyo, Kamati inaamini itakuwa imewasaidia wananchi kupata huduma bora za vivuko.
Mhe. Kakoso ameongeza kuwa Kamati hiyo inathamini kazi kubwa iliyofanywa na Serikali kwa kiwango kikubwa sana hasa miundombinu ikiwemo ya ujenzi wa barabara ambayo imeenea katika jiji la Dar es Salaam kwa kiasi kikubwa.
“Tunampongeza Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa ambazo anazifanya, tunawaomba ninyi kama Wizara mumsaidie kusimamia kukamilisha miradi ambayo imekusudiwa.” Alisisitiza Mhe. Kakoso.
Naye Naibu Waziri wa Ujenzi Godfrey Kasekenya akizungumza na waandishi wa habari amesema kuwa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Miundombinu imewakumbusha kuendelea kuisimamia TEMESA kwa kupeleke fedha haraka za kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya ukarabati wa vivuko, ujenzi wa vivuko vipya pamoja na miundombinu yake ikiwemo majengo ya kupumzikia abiria na maegesho ya vivuko.
“Sisi kama Wizara ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba wananchi hawapati changamoto ya vivuko ama changamoto ya usafiri kwasababu vivuko kwa Wizara ni daraja linalotembea na tunajuwa wana Kigamboni kutokuwepo kwa vivuko kwa muda mrefu maana yake daraja lao halipo kwa muda mrefu ambalo tutahakikisha tunalirejesha muda si mrefu.” Amesema Kasekenya.
Akizungumzia kuhusu fidia kwa wakazi ambao nyumba zao zipo katika eneo la kivuko ambalo linajulikana kwa jina lisilo rasmi la ‘kisambusa’, Naibu Waziri Kasekenya amesema eneo hilo tayari lilitengewa fedha kwa ajili ya kulipia fidia zaidi ya shilingi Bilioni mbili nukta tatu.
“Fidia ile ilishafanyiwa tathmini watu wale waondoke lile eneo litengenezwe liwe la kupaki magari ili kupunguza msongamano wa magari yanayotoka kwenye kivuko ama yanayoingia kwenye kivuko upande ule wa Kigamboni, tayari tulikuwa na mawasiliano ya karibu sana na wenzetu wa Wizara ya Fedha ambao tuna uhakika muda wowote watakapotulipa zile fedha basi na sisi tutaenda kulipa wale watu tuliowafidia ili tuweze kutengeneza mazingira rafiki na bora kwa upande wa Kigamboni ambako tuna uhakika tukishatengeneza lile eneo basi tutakuwa tumepata eneo zuri la maegesho na tutapunguza ule msongamano kama sio kuuondoa kabisa upande wa kule Kigamboni.” Amesema Kasekenya na kuongeza kuwa wabunge ndio wanopanga bajeti na kuidhinisha fedha.
Awali, akijibu baadhi ya maswali yaliyoelekezwa na waheshimiwa wabunge wa kamati hiyo likiwemo suala la ukarabati wa kivuko MV. MAGOGONI, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro Kilahala amesema kivuko MV. MAGOGONI ambacho kilipelekwa mjini Mombasa Kenya kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati mkubwa kinaendelea na ukarabati na kimefikia zaidi ya Asilimia 62%.
“Hivi karibuni tulituma timu kwenda kukagua, kimefika asilimia 62%, baada ya ukaguzi ule mkandarasi amepokea mitambo ambayo tayari ilikuwa imeshaagizwa, injini (engine) na geaboksi (gear box) zimeshakuja wanakamilisha kufunga tutakwenda kukagua tena ili tuwapatie hati nyingine kwa ajili ya kuombea malipo.”
Amesema Mtendaji Mkuu huku akisisitiza kwamba kazi hiyo ya ukarabati inakwenda vizuri.