​BUNGE LAPITISHA BAJETI YA TRILIONI 2.28 KWA WIZARA YA UJENZI

News Image

Posted On: May 07, 2025

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mei 06, 2025 limepitisha kwa kishindo Bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ya Shilingi trilioni 2.28 baada ya mjadala wa kina uliohitimishwa na Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mjadala huo, Waziri Ulega amesema bajeti ya Wizara hiyo imeongezeka kutoka trilioni 1.6 hadi trilioni 2.28, sawa na ongezeko la asilimia 28, hatua ambayo inalenga kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya maendeleo katika Sekta ya Ujenzi.

“Kazi kubwa ya ujenzi katika nchi yetu imefanyika na tunaahidi kuendelea kujenga barabara bila kuchoka, bila kusimama,” alisema Waziri Ulega huku akieleza kuwa wizara hiyo itaendelea kufanya kazi usiku na mchana kutatua changamoto za miundombinu nchini. Katika maelezo yake, Waziri Ulega ameeleza kuwa kuanzia mwaka 2021 hadi sasa, jumla ya Shilingi trilioni 2.5 zimeshalipwa kwa wakandarasi mbalimbali. Pia amebainisha kuwa kila mwezi, Wizara ya Fedha imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kuwalipa wakandarasi wa ndani na nje wanaotekeleza miradi ya barabara.

Aidha, ameeleza kuwa miradi 81 ya dharura yenye thamani ya Shilingi bilioni 559.6 inatekelezwa, ambapo miradi 70 yenye thamani ya bilioni 414 imetekelezwa na wakandarasi wazawa. Katika mwaka wa fedha wa 2024/25, TEMESA ilitekeleza majukumu mbalimbali katika mamlaka yake huku Wakala huo ukikamilisha matengenezo ya magari 19,778 ya serikali, na hivyo kuchangia utoaji wa huduma bila kukatizwa na wizara, idara na Taasisi za Umma. Waziri Ulega alibainisha kuwa matengenezo hayo ni pamoja na siyo magari pekee bali pia mifumo muhimu katika majengo ya Serikali, mifumo ya umeme 114, mitambo ya kielektroniki, 222 ya majokofu na viyoyozi. Kazi hii ya kiufundi, ingawa haionekani sana kwa umma, ni muhimu kwa utendaji kazi wa Taasisi muhimu kama vile hospitali, shule na ofisi za usimamizi.

Pengine mojawapo ya mafanikio yanayoukabili Umma zaidi ya Wakala yapo katika usimamizi wa kivuko, kikoa ambacho TEMESA imekuwa muhimu sana. Kwa mujibu wa Waziri Ulega, shirika hilo kwa sasa linasimamia vivuko 32 vinavyofanya kazi katika maeneo 22 ya kimkakati nchini kote. Katika mwaka uliopita, feri hizi zilisafirisha zaidi ya abiria milioni 18.7, magari 350,000, na zaidi ya tani 103 za mizigo.

“Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya. Hakika hakuna tunachomdai, ameonyesha uongozi wa mfano katika kuimarisha miundombinu ya nchi yetu,” alisema Waziri Ulega.

Katika bajeti hiyo, jumla ya Shilingi 2,280,195,828,000 zimetengwa ambapo Shilingi 90,468,270,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya wizara na taasisi zake, na Shilingi 2,189,727,558,000 zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo.

Bunge limepitisha bajeti hiyo kwa sauti ya pamoja, ikiwa ni ishara ya kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha miundombinu ya usafiri na kuimarisha uchumi wa Taifa.