‘’NIA YETU NI KUONA TUNABORESHA MAISHA YA WATUMISHI KADIRI IWEZEKANAVYO,’’ KILAHALA

News Image

Posted On: November 18, 2024

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Lazaro Kilahala ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuboresha maisha ya watumishi wa Wakala huo hasa katika upande wa maslahi ambapo katika mwaka huu wa fedha wa 2023/2025 Serikali imeajiri watumishi zaidi ya 360 waliokuwa wakifanya kazi kwa mkataba na hivyo kuupunguzia mzigo Wakala huo ambapo iliubidi kutumia mapato yake ya ndani kwa ajili ya kuwalipa watumishi hao mishahara.

Kilahala ametoa shukrani hizo kwa Serikali wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa Makao Makuu wa Wakala huo ambapo amesema hali ya Wakala kiujumla sio mbaya kwa sasa ingawaje hakukuwa na mabadiliko katika kupandisha nauli za vivuko vya Wakala huo pamoja na malipo kabla kwa huduma za karakana.

‘’Tulipata ahueni ya watumishi baadhi kuweza kuingizwa kwenye utaratibu wa kulipwa mishahara na Serikali, jambo ambalo limetupa kidogo ahueni, kwahiyo ile ahueni nadhani tunaiona kwenye maisha ya kila siku, kuna baadhi ya maeneo kidogo vyuma vimelegea naamini sio kama kipindi fulani kilichopita.’’ Amesema Kilahala na kuongeza kuwa Wakala utaendelea kujitahidi na nia kuu kabisa ni kuboresha maisha ya watumishi kadiri iwezekanavyo na kila panapopatikana fursa Wakala utahakikisha fursa hiyo inashuka ikawaguse watumishi wengi hasa wa hali ya chini kwasbabau Taasisi ni ya kwao.

Aidha, Mtendaji Mkuu pia amesema ziko jitihada zimeendelea kufanyika katika eneo la bei za vipuri vya matengenezo ya magari ambapo baadhi ya wadau walitoa maoni kwamba bei za Mikoa zinatofautiana sana, Wakala ulikubaliana na mawazo hayo na kuunda Timu ambayo ilifanya mjumuisho na ulinganifu wa bei zilizolalamikiwa.

‘’Zoezi lile lilifanyika na wazabuni walishirikishwa na ninafahamu kwamba zoezi lilifanikiwa na hatimaye sasa tumefikia hatua ya kuwa na bei ambazo zina ulinganifu, sasa kinachofuata ni kuzipeleka zile bei kwenye Mikoa yetu ili ziweze kutumika sasa katika utekelezaji wa majukumu yetu ya matengenezo ya magari,’’ alisema Kilahala na kuongeza kuwa ni muhimu kufahamu faida ambazo zoezi hilo linakwenda kupeleka kwa Serikali ili kuiona tija yake.

Aidha, akizungumza kuhusu mkakati wa mabadiliko ya Wakala huo, Mtendaji Mkuu amesema suala hilo likikamilika litabadili taswira ya Wakala huo kwa kiasi kikubwa, amesema Serikali imekuwa na maono tofauti ya kutamani kuona TEMESA mpya inapaswa kuwaje, kuna wakati ilitakiwa Sheria ibadilike ili iwe Shirika kutoka kuwa Wakala, lakini pia kulikuwa kuna wazo lingine kwamba sio lazima TEMESA iwe Shirika ndio iweze kuwa na ufanisi, changamoto za Wakala huo zingeweza kutatuliwa bila kubadili Wakala huo kuwa Shirika.

‘’Kwetu sisi tubaki tu na kwamba ziko jitihada zinaendelea kuibadili TEMESA kuwa Shirika , mchakato wa kuibadili kuwa Shirika una hitaji hatua za Kisheria ambazo zina hatua ndefu, lakini mambo yote yale ya msingi yapo, ukizungumzia nauli za vivuko zimo, ukizungumzia suala la malipo kabla limo,ukizungumzia suala la madeni ya TEMESA limo, na kadhalika,’’ alisema Mtendaji Mkuu na kuongeza kuwa tayari wameshampitisha Waziri wa Ujenzi kwenye andiko husika ambapo tayari kuna maboresho ameyaelekeza yafanyike na tayari timu imekwishakamilisha na kuyawasilishakwa ajili ya kufanyiwa maamuzi ya mwisho.

Mtendaji Mkuu meongeza kuwa mabadiliko hayo lazima yatashirikisha wadau wote ikiwemo watumishi wa Wakala huo ambao ndio wahusika wakuu wa mabadiliko hayo.