​WAKAZI TARAFA ZA NYAMIYAGA, RULENGE NGARA KUPATIWA HUDUMA YA KIVUKO

News Image

Posted On: June 21, 2024

Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) inatarajiwa kuanzisha huduma ya kivuko kwa wakazi wanaoishi eneo la Mayenzi kata ya Kibimba Tarafa ya Nyamiyaga na Kanyinya kata ya Mbuba Tarafa ya Rulenge Wilayani Ngara Mkoani Kagera. Wakazi hao wa vijiji vya Mayenzi na Kanyinya, kwa miaka mingi wamekuwa wakitenganishwa na Mto Ruvuvu huku wakitegemea usafiri wa mitumbwi kutoka kijiji kimoja kwenda kingine hali ambayo imekuwa ikihatarisha usalama wao endapo itatokea ajali.

Akizungumza wakati alipofika katika eneo hilo Tarehe 20 Juni, 2024, kukagua kivuko cha MV. RUVUVU pamoja na ujenzi wa miundombinu katika eneo hilo, Mkurugenzi wa Uendeshaji na Ujenzi wa Vivuko kutoka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Mhandisi Sylvester Simfukwe ambaye aliongozana na Mtendaji Mkuu wa Wakala huo Lazaro Kilahala pamoja na wakandarasi wanaosimamia mradihuo, amesema kuwa wamefika eneo hilo kwa ajili ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ambayo itatumika mara baada ya huduma za kivuko eneo hilo kuanza ikiwemo ujenzi wa jengo la kupumzikia abiria, ujenzi wa jengo la choo, jengo la kukatisha tiketi pamoja na ujenzi wa maegesho ya kivuko.

Mhandisi Simfukwe amesema Serikali imeamua kupeleka kivuko katika eneo hilo kiweze kutumika kuvusha wananchi wa Tarafa ya Rulenge na Tarafa ya Nyamiyaga na kusema kuwa kivuko hicho kitawasaidia wananchi kutoka upande wa kijiji cha Kanyinya kufika kwa urahisi eneo la Ngara mjini kwa ajili ya kujipatia huduma mbalimbali za kijamii tofauti na hapo awali ambapo iliwalazimu kuzunguka umbali mrefu kufuata huduma hizo za kijamii ama kuvuka kwa kutumia mitumbwi midogo ya mbao ambayo ilihatarisha usalama wao.

‘’Kwa muda mrefu wananchi wa huku hawakuwa na huduma ya kivuko, mara kivuko hiki kitakapofunguliwa watakuwa wanapata huduma ya kuvuka badala ya kutumia mitumbwi ambayo kwakweli si salama sana,’’ amesema Mhandisi Simfukwe huku akiongeza kuwa TEMESA inaanza kukifanyia ukarabati mzuri kivuko hicho ili ndani ya miezi miwili mpaka mitatu kiweze kuanza kutoa huduma.

‘’Kuna mikakati tumeiweka ili kukifanya kivuko hiki kiweze kutoa huduma kwa wananchi, mikakati hiyo ni pamoja na kuja kukifanyia marekebisho makubwa kwasababu kimekaa muda mrefu hapa, tutakuja kukipaka rangi ambayo ni maalumu kwa ajili ya vivuko, tutaondoa kutu, halafu pia tutakifunga nyaya za kukiendeshea pamoja na kukifunga injini moja ya nje yenye uwezo wa hozi pawa arobaini (40) ambayo itaweza kutekeleza hili jukumu bila matatizo yoyote.’’ Amesema Mhandisi Simfukwe huku akiongeza kuwa ana imani wananchi wa maeneo hayo watafurahia huduma ya kivuko ndani ya muda mfupi ujao ambayo haikuwahi kuwepo eneo hilo.

Naye Mkandarasi anayesimamia ujenzi wa miundombinu katika eneo hilo la kivuko Bwana Emmanuel Ikula, akizungumza mara baada ya ukaguzi huo amesema, mpaka sasa mradi huo tayari umefikia zaidi ya asilimia themanini na tano (85%) na wanatarajia ndani ya mwezi mmoja majengo yote yatakuwa tayari yamekamilika.

‘’Tunategemea majengo yeu yataweza kukamilika ndani ya mwezi mmoja, kwasababu tumebakiza vitu vichache, vyoo vimeshajengwa, sakafu zimeshajengwa na kuwekwa tailizi, milango imekwishawekwa, madirisha, kwahiyo sasa hivi ni umaliziaji tu wa kuwezesha ofisi ziweze kufanya kazi na tunatumaini ndani ya siku thelathini tutakuwa tumeshakamilisha kwa ajili ya matumizi ya kiofisi kuweza kuendelea.’’Alisistiza Bwana Ikula.

Kivuko cha MV. RUVUVU kina uwezo wa kubeba abiria sitini (60) na magari mawili (2) na hapo awali kilikuwa kinatoa huduma eneo la Rusumo na Nyakiziba Wilayani Ngara Mkoani Kagera. Kivuko hicho kinategemewa kwenda kuchochea shughuli za kimaendeleo kati ya wanavijiji wa kata hizo na kuboresha hali zao za kiuchumi.