MTENDAJI MKUU MPYA TEMESA AKABIDHIWA OFISI RASMI

News Image

Posted On: December 15, 2021

Bi. Monica A. Moshi, leo amekabidhiwa rasmi ofisi na vitendea kazi vyote kutoka kwa Mtendaji Mkuu aliyemaliza muda wake Mhandisi Japhet Y. Maselle katika ofisi za makao makuu ya Wakala wa Ufundi na Umeme nchini yaliyopo mjini Dodoma.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Kaimu Mtendaji Mkuu aliyeachiwa ofisi, Monica A. Moshi, amemshukuru Mhandisi Maselle kwa muda wote ambao amefanya kazi chini yake na kumpongeza kwa kazi nzuri aliyoifanya muda wote ambao ameutumikia Wakala huo kwa zaidi ya miaka thelathini.

‘’Ametufundisha mambo mengi sana kwa kipindi kifupi, lakini mimi ninaamini kwamba tutaendelea kumtumia kwa muda wote ambao TEMESA itaendelea kuwepo, nakushukuru sana, tunakuombea utumishi mwema huko unakoenda’’, alisema Mtendaji Mkuu mpya na kuahidi kuwa watumishi wataendelea kusaidiana katika kazi, kufanya kazi kwa bidii, kutoweka makundi, kutofanya kazi wakiwa na hasira na kutoonea watumishi wengine.

Naye Mtendaji Mkuu ambaye amemaliza muda wake Mhandisi Japhet Y. Maselle, akizungumza wakati wa makabidhiano hayo ameushukuru Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA kwa kumpa ushirikiano wa kutosha muda wote ambao amefanya nao kazi na kuwaomba kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa huku akiwasisitizia ushirikiano kwa kila mmoja.

‘’Hakikisha unashirikiana na kila mmoja, moja la msingi sana msiwe na makundi, kusiwe na makundi katika utekelezaji kwasababu mkiwa na makundi mtakua mnavutana, kuweni kitu kimoja, TEMESA ni yetu na na uhakika mtafika mbali’’, alimaliza Mhandisi Maselle na kuwatakia kila laheri watumishi wa menejimenti ya TEMESA walioshiriki makabidhiano hayo.