KIVUKO KIPYA MWAROBAINI WA CHANGAMOTO UKEREWE
Posted On: August 05, 2024
Meneja wa Vivuko Kanda ya Ziwa na Magharibi, Mhandisi Vitalis Bilauri amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha TEMESA kujenga kivuko kikubwa kitakachotatua changamoto za wananchi wa Rugezi Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza na Kisorya Wilayani Bunda Mkoani Mara.
Mhandisi Bilauri amezungumza hayo wakati alipotembelea kivuko cha Kisorya – Rugezi kujionea namna vivuko vinavyotoa huduma kwa wananchi eneo la Kisorya - Rugezi ambapo amewatoa hofu wananchi wa maeneo hayo kwa changamoto wanazokutana nazo pindi wanapopata huduma na amewaahidi kuwa hivi karibuni zitapatiwa utatuzi.
Mhandisi Bilauri amesema kwa kiasi kikubwa, wakazi wa Ukerewe na Bunda wanategemea vivuko katika shughuli zao za kiuchumi kwakuwa sehemu kubwa ya eneo hilo imezungukwa na ziwa hivyo basi huduma zao zimekuwa zikitegemea sana vivuko vitatu ambavyo ni MV. UJENZI, MV. UKARA II pamoja na MV. ILEMELA.
“Tunafahamu kabisa kwa wakazi wa huku maisha yao yanategemea vivuko kwa sababu Ziwa limewazunguka na kwa kutambua hilo huduma zetu juu ya kisiwa hiki na wakazi walioko hapa tuna vivuko vitatu ambavyo tunaviendesha”, alisema Meneja huyo na kuongeza kuwa wananchi hao kupitia vivuko, maisha yao na shughuli zao za kibiashara na kiuchumizimerahisishika kwa sababu muda wote wanavuka na vivuko vimekuwa msaada mkubwa sana kwao.
Aidha, Mhandisi Bilauri amesema idadi ya watu katika maeneo hayo imekua ikiongezeka siku hadi siku na Serikali imeona changamoto wanazozipata wananchi kutokana na ufinyu wa vivuko na imeamua kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kivuko kingine kipya chenye uwezo wa kubeba abiria mia nane na magari ishirini na mbili.
Mhandisi Bilauri amesema mpaka sasa kivuko hicho kinaendelea kujengwa na kipo kwenye hatua za mwisho za matengenezo hivyo basi wananchi wasiwe na wasiwasi sababu ufumbuzi wa changamoto zao tayari umepatikana.