Ujenzi wa kivuko kipya Kigongo – Busisi Mwanza kukamilika mwezi Mei 2018

News Image

Posted On: March 22, 2018

Wakazi wa jiji la Mwanza wanatarajia kuanza kupata huduma ya kivuko kipya ndani ya miezi miwili ijayo kinachojengwa na mkandarasi wa kizalendo jijini humo.

Ujenzi wa kivuko hicho ambacho kitatoa huduma zake kati ya Kigongo na Busisi katika Ziwa Victoria unatarajiwa kukamilika mwezi Mei mwaka huu.

Kivuko hicho kipya kinachojengwa na kampuni ya kizalendo ya Songoro Marine Transport Boat Yard ya jijini Mwanza umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 8.9 za Kitanzania na kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kubeba abiria 1000, magari 36 na kitakua na Tani 250.

Akizungumza mbele ya Kamati ya Bunge ya Miundombinu ambayo ilitembelea kukagua maendeleo ya ujenzi huo katika yadi ya Songoro iliyopo Ilemela, Meneja wa masuala ya fedha wa kampuni ya Songoro. Ndugu Mohamed Salum alisema kivuko hicho kilitakiwa kuwa tayari kimeanza kutoa huduma lakini kutokana na urasimu kimechelewa kuanza kutoa huduma.

Meneja huyo pia alitaja ucheleweshwaji wa malipo kutoka serikali kuu, kukatika kwa umeme mara kwa mara na kunyesha kwa mvua mfululizo kama changamoto nyingine ambazo zimechelewesha kukamilika mapema kwa mradi huo. Aliihakikishia kamati hiyo kuwa, asilimia 25 zilizobakia kukamilisha ujenzi huo zitamalizika mwezi Mei na kivuko hicho kitakabidhiwa kwa Serikali kuanza kutoa huduma.