VIVUKO VIPYA KUANZA KUKAMILIKA KUANZIA SEPTEMBA MWAKA HUU

News Image

Posted On: June 18, 2024

Ujenzi wa vivuko vipya vitano vinavyoendelea kujengwa na Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Mkoani Mwanza chini ya Mkandarasi kampuni ya Songoro Marine, unatarajiwa kuanza kukamilika ifikapo mwezi Septemba mwaka huu. Vivuko hivyo vipya vitakapokamilika vitakwenda kutoa huduma kati ya maeneo ya Ijinga na Kahangala Wilayani Magu, Bwiro na Bukondo Wilayani Ukerewe, Nyakaliro na Kome Wilayani Sengerema, Buyagu na Mbalika Wilayani Sengerema pamoja na Kisorya Wilayani Bunda Mkoani Mara na Rugezi Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza.

Hayo yamebainishwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala, Lazaro kilahala wakati alipotembelea Yadi ya kampuni hiyo iliyopo Ilemela Mkoani Mwanza kukagua maendeleo ya ujenzi wa vivuko hivyo leo Tarehe 18 Juni, 2024.

Akizungumza mara baada ya kujionea ujenzi unavyoendelea, Kilahala amesema ameridhishwa na Maendeleo ya ujenzi wa vivuko hivyo na asilimia ambazo umefikia ujenzi huo, ‘’tumeridhishwa na maendeleo, mara ya mwisho tulikuwa hapa mwezi Mei ambapo kivuko kama Buyagu Mbalika kilikuwa kwenye asilimia 45%, leo hii tumekuja hapa kimeshafika asilimia 75%, kivuko kama Nyakarilo Kome kilikuwa kwenye asilimia 60%, na chenyewe sasa hivi kimefika kwenye asilimia 75%, kwahiyo tunamshukuru mkandarasi anaendelea kupambana kuhakikisha kwamba kazi inasogea’’. Amesema Mtendaji Mkuu na kuongeza kuwa kwa mujibu wa mpango kazi, vivuko hivyo vinategemewa kuanza kukamilika mwezi Septemba mwaka huu endapo kila kitu kitaenda kama kilivyopangwa.

Mtendaji Mkuu amesema kuwa kwa wastani vivuko vya Buyagu na Mbalika pamoja na Nyakarilo Kome vimefikia wastani wa asilimia 75% za ujenzi wake, wakati vivuko vya Ijinga Kahangala, Kisorya Rugezi na Bwiro Bukondo kwa wastani vimefika Zaidi ya asilimia 85% ya ujenzi wake.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Major Songoro, akizungumza mara baada ya ukaguzi huo, amesema kuwa, kuanzia mwezi wa Tisa mwaka huu, baadhi ya vivuko vitakuwa tayari vimekamilika na vitatolewa kwa ajili ya kwenda kutoa huduma katika maeneo ambayo vimepangiwa.

Songoro amesema kuwa vivuko hivyo viko katika hatua mbali mbali za ujenzi, ikiwemo vingine kuanza kufungwa injini ambapo amesema vivuko viwili tayari vimekwishafungwa injini, gia boksi, shafti, propela na mifumo ya umeme huku vivuko vingine vikiendelea kufungwa mifumo mingine ikiwemo mabomba ya maji, mifumo ya kupambana na dharura ya moto pamoja na mifumo ya pampu za haidroliki. Songoro ametoa shukran za dhati kwa Serikali kwa kuwapatia fursa wakandarasi wazawa ya kujenga vivuko hivyo huku akiahidi kukamilika kwa wakati ujenzi wa vivuko hivyo.