MKUU WA MKOA MWANZA AIPONGEZA SERIKALI KWA UWEKEZAJI MKUBWA ZIWA VICTORIA
Posted On: September 17, 2025
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa uwekezaji mkubwa inaoendelea kuufanya katika Ziwa Victoria ikiwemo kuboresha huduma za usafiri wa vivuko. Mhe. Mtanda ameyasema hayo TAREHE 16 Septemba, 2025 wakati alipokuwa akishuhudia kivuko MV. BUKONDO kikishushwa kwenye maji kwa ajili ya kuanza kufanyiwa majaribio baada ya ujenzi wake kukamilika.
Mkuu wa Mkoa aamesema kuwa mradi huo wa ujenzi wa kivuko MV. BUKONDO ni mradi mkubwa na unaenda kuepusha ajali ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara katika visiwa hivyo kutokana na wananchi hao kukosa huduma ya uhakika ya usafiri hali ambayo inawalazimu kutumia mitumbwi midogo na boti za mbao ambazo sio salama kwa ubebaji wa mizigo na abiria wanaosafiri masafa marefu.
Mhe. Mtanda pia ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa kutekeleza miradi ya usafiri wa maji kwa wakazi wa Mkoa wa Mwanza, ‘’kwahiyo kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Mwanza, nichukue fursa hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri aliyoifanya na kwa uwekezaji mkubwa alioufanya ndani ya Ziwa Victoria,’’ amesema Mtanda na kuendelea kumpongeza Mhe. Abdallah Ulega, Mtendaji Mkuu wa TEMESA pamoja na mkandarasi Songoro Marine ambaye amejenga kivuko hicho na vingine.
Naye, Mkurugenzi wa Uendeshaji na Ujenzi wa Vivuko TEMESA mhandisi Lukombe King’ombe akizungumza wakati wa tukio hilo amesema kivuko cha MV. BUKONDO ambacho kimeshushwa kwenye maji kina uwezo wa kubeba tani 100, abiria 200 pamoja na magari madogo 10. Mhandisi King’ombe ameongeza kuwa baada ya zoezi la kushusha kivuko MV. BUKONDO, kivuko kitakachofuatia kushushwa kwenye maji ni MV. UKEREWE. Amesema kuwa kivuko cha MV. UKEREWE ambacho kitakwenda kutoa huduma kati ya Kisorya Wilayani Bunda Mkoani Mara na Rugezi Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza, kina uwezo wa kubeba tani 170, abria 800 pamoja na magari 22 na kuongeza kuwa vivuko vyote vimejengwa kwa kuzingatia sheria za kimataifa za ujenzi wa vyombo vya maji.
‘’Vivuko hivi vyote vinavyojengwa hapa vimezingatia ubora wa vifaa vyote ambavyo vinahitajika kwenye vyombo vya majini, vyombo hivi ni vya kisasa vina vifaa vyote vya kuongozea meli vya kisasa, kwahiyo tunatarajia wananchi katika maeneo husika watapata huduma wanayoitarajia kutokana na ujio wa vivuko hivi.’’ Alisema Mhandisi King’ombe.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Marine, Major Songoro akziungumza na waandishi wa habari amesema kuwa tukio hilo ni tukio kubwa na la furaha kwa kampuni hiyo kuweza kumaliza ujenzi wa kivuko hicho pamoja na vivuko vingine na ni hatua kubwa ambayo inapaswa kupongezwa. Ameipongeza Serikali, Wizara ya Ujenzi pamoja na TEMESA kwa kuweza kufanikisha ukamilishaji wa mradi huo huku akiwaasa wakazi wa Bukondo na Bwiro kuendelea kutoa shukrani kwa Serikali kwakuwa inafanya kazi kubwa kuhakikisha wakazi hao wanapata usafiri wa uhakika.
‘’Serikali kwa kweli inapiga kazi kubwa sana, kwahiyo wakazi wa Bukondo wawe na imani na Serikali yao ukiangalia hiki chombo pesa nyingi sana imeingia kujenga hiki chombo’’, amesema Songoro na kuendelea kumpongeza Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kujenga Taifa na kuboresha miundombinu ya usafiri wa maji.