KIVUKO CHA MV.TEMESA CHAREJEA KUTOA HUDUMA

News Image

Posted On: April 17, 2022

Kivuko cha MV. TEMESA kinachotoa huduma kati ya Ilunda Wilayani Sengerema na Luchelele Wilayani Nyamagana tayari kimerejea kutoa huduma kwa wakazi wa maeneo hayo wanaoutumia usafiri wa maji katika Ziwa Victoria baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa uliochukua takribani miezi miwili. Kivuko hicho kimefanyiwa ukarabati mkubwa na kampuni ya Ms. Songoro Marine katika yadi yake iliyopo Ilemela Mkoani Mwanza. Akizungumza na mwanahabari, Kaimu Mkuu wa Kivuko cha MV. TEMESA, Lucas Mahuma amesema chombo hicho baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa, sasa kinaendelea kutoa huduma kama kawaida ambapo alitaja pia ratiba ya kivuko hicho ambapo amesema kinafanya kazi mara tatu kwa siku ambapo ameeleza kuwa, kinavusha abiria kuanzia saa mbili na nusu asubuhi, saa saba kamili mchana na kumalizia saa kumi na mbili za jioni na baada ya hapo kinapumzika. Nao baadhi ya wakazi wa maeneo ya Ilunda na Luchele wanaotumia kivuko hicho kwa shuguli zao za kila siku hasa wafanyabiashara wa mkaa na biashara za mazao, wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi hao ambao wanategemea kivuko hicho kwa usafiri wa kila siku, wamesema kipindi chote ambacho kivuko hicho kilikuwa kwenye ukarabati, walikuwa wakipata shida kubwa ya usafiri hali iliyowalazimu kutumia usafiri wa mitumbwi midogo ambayo ilikuwa ikihatarisha usalama wa maisha yao na bidhaa zao za kibiashara walizokuwa wakisafirisha kupitia usafiri wa mitumbwi. Wakazi hao wameishukuru Serikali kwa kuweza kukamilisha ukarabati huo kwa wakati kwani sasa wameanza kurudi kutumia usafiri huo ambao ni wa uhakika na salama zaidi kwa maisha yao pamoja na bidhaa zao ambazo wamekuwa wakizisafirisha kwa kutumia kivuko hicho tangu awali. Wakazi hao pia kwa nyakati tofauti wameiomba Serikali kukamilisha ujenzi wa maegesho mapya katika eneo la Ilunda Wilayani Sengerema kutokana na maegesho hayo kutokuwa kamilifu na hivyo kukilazimu kivuko hicho kupaki eneo ambalo sio sahihi hali inayosababisha kishindwe kubeba magari kutokana na magari hayo kushindwa kupata njia sahihi ya kuingilia ndani ya kivuko. Kivuko cha MV. TEMESA kina uwezo wa kubeba abiria 80 pamoja na magari 5 sawa na tani 65. #Sensayawatunamakazi2022JiandaeKuhesabiwa

Tanzania Census 2022