UKARABATI MV. MAGOGONI WAFIKIA ASILIMIA 40%

News Image

Posted On: January 30, 2024

Ukarabati wa kivuko MV. MAGOGONI unaoendelea huko mjini MOMBASA Kenya sasa umefikia asilimia 40%. Hayo yamebainishwa Tarehe 28 Januari 2024 na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro Kilahala wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwa ajili ya kuwapa taarifa kuhusu maendeleo ya ukarabati wa kivuko hicho pamoja na mipango ya muda mrefu na mfupi na mikakati ya Wakala huo katika kuhakikisha huduma za vivuko katika eneo la Magogoni Kigamboni na maeneo mengine yote Nchini unaimarika.

Kilahala amesema kuwa Wakala una mipango ya namna mbili ambayo ni ya muda mfupi na ya muda mrefu huku akitanabaisha kuwa mipango ya muda mfupi ni pamoja na kukodi Sea Taxi, vivuko vidogo viwili kutoka kampuni ya Bakhresa ambavyo vinaendelea kusaidiana na vivuko vilivyobakia katika eneo la Magogoni Kigamboni kutoa huduma kwa wakazi wa maeneo hayo pamoja na mpango wa muda mrefu ambao ni kuhakikisha kivuko MV. MAGOGONI kinamalizika kufanyiwa ukarabati mkubwa na kurejea kutoa huduma kwa haraka zaidi.

''Tunafahamu kwamba huu mradi umechukuwa muda mrefu zaidi ya tulivyotarajia, kulikuwa na changamoto za hapa na pale za kiutendaji lakini tunashukuru kwamba zimekwishatatuliwa, sasa hivi hiki kivuko kiko kwenye ukarabati kimefika wastani wa asilimia 40%.’’ Amesema Mtendaji Mkuu na kuongeza kuwa TEMESA kwa sasa inataka kuongeza nguvu kwakuwa changamoto zote sasa zimekwishaanza kutatuliwa ili kuhakikisha ukarabati huo unakamilika kwa wakati na kuondoa kero iliyokuwepo.

Mtendaji Mkuu amesema kwakuwa vivuko MV. KAZI NA Sea Taxi kwa sasa vinafanya kazi peke yake na haviwezi kutoa huduma ya uhakika, kutokana na sababu hiyo, Serikali inafanya mikakati ya makusudi kuhakikisha kivuko MV. KIGAMBONI kinafanyiwa ukarabati mdogo wa mara kwa mara ili kuhakikisha raia wanaendelea kupata huduma ya uhakika wakati kikisubiri kivuko MV. MAGOGONI kukamilika na kurejea kwa ajili ya kukitoa MV. KIGAMBONI kwenye maji na kupelekwa kwenye ukarabati mkubwa. Kilahala ameongeza kuwa Serikali imeanza mchakato wa kutengeneza Sea Taxi nyingine mbili ambazo zitaenda kutoa huduma katika eneo hilo ili kurahisisha huduma ya usafiri.

Naye Meneja wa Vivuko Kanda ya Mashariki na Kusini Mhandisi Lukombe King’ombe akizungumzia kuhusu kivuko MV. KIGAMBONI ambacho kimesimama kutoa huduma kutokana na kuharibika kwa mfumo wake wa uendeshaji, amesema tayari wameagiza vipuri ambavyo vinatarajiwa kuwasili kuanzia Tarehe 30 Januari 2024. ‘’Vipuri hivyo vimetumwa kwa njia ya ndege kutoka Uholanzi na ni vipuri kwa ajili ya huo mfumo wa uendeshaji wa kivuko chetu cha MV. KIGAMBONI, kwahiyo vipuri vitakapofika mara moja timu yangu ya ufundi itafunga vipuri hivvo na tunaamini hatuwezi tukachukua zaidi ya wiki kivuko kitarudi kwenye utendaji wake na tutawaita wenzetu wa TASAC kwa ajili ya kukikagua na kukiruhusu kiendelee kutoa huduma.’’ Amesema Mhandisi King’ombe.