UKARABATI MKUBWA MV. MAGOGONI WAFIKIA HATUA NZURI
Posted On: March 12, 2024
Ukarabati mkubwa wa kivuko MV. MAGOGONI unaoendelea Mombasa Nchini Kenya umefikia hatua nzuri, ukarabati huo mkubwa unaojumuisha ununuzi na uwekaji wa mitambo yote mipya ya uendeshaji wa kivuko zikiwemo injini mpya na mitambo yake, uwekaji wa mabati mapya ya kivuko pamoja na vifaa vyote vya uongozaji wa kivuko, unafanywa na kampuni ya African Marine iliyoko eneo la Tangana, Mbaraki Mombasa Nchini Kenya.
Akizungumza wakati akikagua maendeleo ya ukarabati wa kivuko hicho leo, Kaimu Mkurugenzi wa Ujenzi na Matengenezo ya Vivuko kutoka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Mhandisi Sylvester Simfukwe amesema, kwa sehemu kubwa wameweza kuona Mkandarasi alipofikia kwenye kazi ya ukarabati huo na kusema kuwa kumekuwepo na maeneo ambayo yaliwahitaji wataalamu kufika ili kuhakiki baada ya kivuko kuwa kimetolewa kwenye maji na kuinuliwa juu, wao kama wataalamu wamefika na kujionea na watatoa mapendekezo yao ili kuweza kuhakikisha kazi hiyo inafanyika kwa ukamilifu.
‘’Kuna vitu vingine ambavyo vilikuwa si rahisi kuonekana wakati wa ukaguzi wa awali, sasa wakati kikiwa juu tumeweza kujionea maeneo mbalimbali yakiwemo mabati ya kivuko (marine plates) ambayo yamechakaa sana na yako nje ya ule ubora unaotakiwa.’’ Amesema Mhandisi Simfukwe na kuongeza kuwa mitambo ya uendeshaji wa kivuko hicho pia ilikuwa inahitaji wataalamu (OEM) ambao ndio watengenezaji halisi wa mitambo hiyo na baada ya kufika na kuifanyia majaribio, wamegundua mitambo hiyo haiwezi ikafaa kuendelea kutumika.
‘’Tumeona maeneo mengine kama yale ya mifumo ya kuendeshea kivuko (Propulsion Units), mifumo ya pampu jeti ambayo ndio inatumika katika hiki kivuko, mafundi wakati wa ukaguzi wa awali kwasababu yako chini ya maji, wasingeweza kabisa kujua uharibifu ulioko ndani, lakini baada ya kuyabomoa tumekuta vifaa hivyo vimekwishaharibika mno kiasi kwamba huwezi kuyarudishia, haya yote tumeona ni lazima yafanyike na yanaweza kua na gharama ambazo zitaongezeka, lakini ni ili kivuko chetu kikafanye kazi kwa muda mrefu na kwa ufanisi zaidi.’’ Amesema Mkurugenzi na kuongeza kuwa watayashauri kwa ngazi husika za juu ili yaweze kufanyiwa mabadiliko ya kimkataba ili Mkandarasi African Marine aweze kufanya na kumaliza kazi yake kwa wakati.
Kaimu Mkurugenzi ameongeza kuwa wao pamoja na Mkandarasi na Mshauri Elekezi wa Mradi huo Chuo cha Bahari Nchini (DMI), wanaendelea kufanya majadiliano ili kuhakikisha vyote ambavyo vimeongezeka na vinastahili kubadilishwa vinafanyiwa utaratibu na kupelekwa ngazi za juu kwa ajili ya kufanyiwa kazi
Halikadhalika, Mkurugenzi wa Kampuni hiyo inayoendesha ukarabati huo mkubwa Sabareesan Asokan, akizungumza mara baada ya ukaguzi amesema, kwa sasa wanasubiria kuwasili kwa injini na mitambo mingine ya uendeshaji wa kivuko hicho ambayo imeagizwa kutoka nje ya Nchi ili waweze kuanza kuifunga.
‘’Kwa sasa tunasubiria injini na vifaa vingine vifike, tunategemea viwasili muda si mrefu kutoka nje ya Nchi na tunategemea kumaliza ukarabati huu ndani ya muda.’’ Amesema Mkurugenzi wa Kampuni hiyo.
Naye Mhandisi wa Mitambo ya Meli Lazaro Isack Lazaro kutoka Chuo cha Bahari Nchini (DMI) ambao ndio washauri elekezi wa mradi wa ukarabati wa kivuko hicho, akizungumza mara baada ya kufanya ukaguzi huo amesema kama washauri, wamejionea kazi kubwa ambayo tayari imefanyika na wanatarajia ndani ya muda mfupi ukarabati huo utakamilika. Mhandisi Lazaro amesema wao kama washauri elekezi, watatumia utaalamu wao kuishauri Serikali vizuri na kuhakikisha wanasimamia thamani ya fedha inayotengwa ili itumike kwa usahihi kwa ajili ya ukarabati huo.
Msimamizi wa Ujenzi na Matengenezo ya Vivuko kutoka TEMESA Mhandisi Faustine Malunde Kachwele naye akizungumza, amesema kuwa wao kama wasimamizi wa mradi huo kwa kushirikiana na Chuo cha Bahari Nchini (DMI), watahakikisha ukarabati huo unafanyika kwa ubora kwa kuzingatia Sheria za maji zinazoongoza vyombo hivyo ili kivuko hicho kirejee na kitoe huduma yenye ubora kwa wakazi wa Kigamboni.
Kivuko MV. MAGOGONI chenye uwezo wa kubeba abiria 2000 na magari 36 kinatoa huduma kati ya Magogoni na Kigamboni jijini Dar es Salaam na ni mojawapo ya vivuko vikubwa hapa Nchini ambacho kinategemewa kwa kiasi kikubwa katika utoaji huduma eneo hilo kutokana na uwezo wake mkubwa wa kubeba abiria na magari mengi kwa wakati mmoja.