TEMESA YAKAMILISHA MATENGENEZO KIVUKO MV. KILAMBO

News Image

Posted On: August 09, 2024

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara Bi. Bahati Geuzye, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha TEMESA kukifanyia matengenezo kivuko cha MV. KILAMBO kilichokuwa kinasaidia kutoa huduma eneo la Lindi – Kitunda mara baada ya kivuko MV. KITUNDA kinachotoa huduma eneo hilo kuondolewa kwenye maji kwa ajili ya kufanyiwa ukarabati mkubwa.

Akizungumza na vyombo vya Habari leo tarehe 09 Agosti 2023, Bi.Geuzye ambaye aliongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mtwara, amesema kuwa wamefika eneo hilo kwa ajili ya kukagua matengenezo yaliyofanyika kwenye kivuko hiko ambapo pia amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Lindi kwa kuwapa ridhaa ya kufanya ukaguzi kwenye kivuko hiko.

Bi. Geuzye amesema wametembelea kukagua na wameona namna TEMESA imefanya matengenezo makubwa hasa kwenye upande wa injini, kurekebisha vipuri mbalimbali na kukiboresha kivuko hiko na kuwahakikishia wananchi kuwa hivi karibuni kitaenda kutoa huduma mpakani mwa Mtwara eneo la Kilambo na Namoto.

“Tumeweza kutembelea na kukagua matengenezo ambayo yamefanywa na Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA na tumeona wamefanya matengenezo makubwa katika injini ya kivuko hiki na pia vipuri mbalimbali wameweza kuvirekebisha na kuviboresha kwa ujumla kivuko kinaonekana kiko katika hali nzuri,” amesema Katibu Tawala.

“Wameweza kutuwashia hata injini hizo, tumeona zinavyofanya kazi na kuna matengenezo madogo wanaendelea nayo, wametuhakikishia kuwa sasa kivuko kiko tayari kurudishwa Mtwara ambapo kitafanya kazi katika mpaka wetu wa Kilambo ili kiweze kusaidia wananchi”, Alisistiza Bi Geuzye.

Naye Mkuu wa Matengenezo TEMESA Kanda ya Mashariki na Kusini, Mha. Reuben Mataru amesema wamefanya matengenezo makubwa yatakayosababisha kivuko kiwe na uhakika wa kutumika mda mrefu bila kuharibika.

“Vifaa vingi sana vimebadilishwa, injini zimefanyiwa marekebisho makubwa na kilitokea toka mwaka 2009, 2010 ndio kilikuja na kimefanyiwa marekebisho makubwa ya ijnini namba moja na kilikamilika rasmi na kwa matengenezo ya sasa na siku ya jumamosi tukaanza kufanya majaribio ya kuvusha hadi siku ya jumanne, jumatano tukaanza kukifanyia usafi kwa ajili ya kukikabidhi”, Alisisitiza Mha. Reuben.

Kivuko cha MV. KILAMBO kina tani 50 na kina uwezo wa kupakia abiria 100 na magari matatu.