MV. KIGAMBONI YAREJEA MAGOGONI

News Image

Posted On: May 30, 2020

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe leo amepokea Kivuko cha MV Kigamboni kilichokuwa kinafanyiwa ukarabati mkubwa katika eneo la Kigamboni jijini Dar es salaam. Ukarabati huo uliogharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.09 zilizotolewa na Serikali ya Tanzania umefanywa na kampuni ya kizalendo ya Songoro Marine Transport Boatyard katika yadi yake iliyopo Kigamboni.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhandisi Kamwelwe alimshukuru Mheshimiwa Rais Dk. John Pombe Magufuli kwa kuendelea kukamilisha ahadi za miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi.Pia alitoa wito kwa watumishi wa TEMESA kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha Kivuko cha MV Kigamboni pamoja na Vivuko vingine vinatuzwa na kufanyiwa matengenezo kinga mara kwa mara ili viendelee kudumu.

Aidha alisema ununuzi wa Vivuko na Boti peke yake katika kipindi cha kuanzia Novemba 2015 hadi sasa umeigharimu Serikali kiasi cha shilingi bilioni 38.6 na kufanya Wizara yake iweze kutekeleza ilani ya uchaguzi ya chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Maselle alisema kivuko cha MV Kigamboni kilianza kujengwa Disemba 2018 na kukamilika Mei 6 mwaka huu. Kivuko cha MV Kigamboni kina uwezo wa kubeba tani 160, magari madogo 22 na abiria 800 kwa wakati mmoja.Pia Kivuko hicho kina urefu wa mita 52, upana mita 12.

“Kivuko hiki kimefanyiwa ukarabati mkubwa kwa kubadilisha vifaa vya kujiokolea kwa kuweka life jackets mia nane kwa ajili ya wakubwa na themanini kwa ajili ya watoto pamoja na maboya,” alisema Mhandisi Maselle.

Mhandisi Maselle alisema ukarabati wa Kivuko umekamilika kulingana na viwango vya Kimataifa(IMO Standards) na ukaguzi umefanywa na Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) na kudhibitisha kivuko hiki ni salama kwa ubebaji wa abiria, magari na mizigo.

“Kukamilika kwa Kivuko hicho kunarudisha idadi ya vivuko vitatu katika kituo cha Magogoni na hivyo kuondoa adha ya usafiri iliyokuwepo kwa wananchi wakati kilipokuwa kinafanyiwa matengenezo,’’alisema Mhandisi Maselle.

Mapokezi ya kivuko hicho yalihudhuriwa na Mbunge wa Kigamboni Faustine Ndugulile, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Bi Sarah Msafiri, viongozi waTEMESA makao makuu na mkoa wa Dar es salaam pamoja na wananchi wanaotumia Vivuko hivyo.