MV.KAZI KUREJEA ALHAMISI IJAYO
Posted On: November 29, 2022
Kivuko cha MV. KAZI kinachofanyiwa ukarabati mkubwa katika Yadi ya Songoro iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam sasa kitarejea kwenye maji siku ya Alhamisi Tarehe 8 Desemba mwaka huu, hayo yamebainishwa na Meneja wa Vivuko Kanda ya Mashariki na Kusini Mhandisi Lukombe King’ombe wakati akifanya mahojiano maalumu na mwandishi kutoka Televisheni ya Taifa (TBC), mahojiano yaliyofanyika katika Yadi ya matengenezo ya kampuni hiyo mapema leo asubuhi ambapo alipata pia wasaa wa kukagua maendeleo ya ukarabati huo.
Mhandisi King’ombe amesema kivuko hicho tayari kimeshafungwa milango mipya (ramps), mashine mpya za kusaidia milango hiyo kunyanyuka kwa ajili ya kuruhusu magari na abiria kupita, kimewekewa pia maboya mapya ya kujiokolea zaidi ya 880 kwa ajili ya abiria, mhandisi King’ombe pia amesema kivuko hicho tayari kimefungwa injini zote mpya na kwa sasa kinachosubiriwa ni kuwashwa kwa injini hizo kabla ya kukishusha kwenye maji kwa ajili ya kukifanyia majaribio ili kianze kutoa huduma.
‘’Matarajio yetu ni tumemwelekeza mkandarasi, baada ya kulipwa malipo ya awali kwa mujibu wa mkataba alitakiwa amalize kazi hii ndani ya wiki 20 na hizi wiki 20 zinaisha Tarehe 30 ya mwezi Novemba, kwahiyo yupo kwenye hatua za mwisho kwa ajili ya kukamilisha mradi huu na tunatarajia ashushe kivuko hichi kwenye maji ifikapo wiki ijayo na kitakaposhushwa sasa kwenye maji wenzetu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania ambao wanasimamia vyombo vya majini (TASAC) watafanya ukaguzi wao na kutupa cheti kwa ajili ya kukirudisha sasa chombo kianze kutoa huduma kwa wananchi wa Kigamboni’’. Alimaliza Mhandisi King’ombe na kuongeza kuwa TEMESA inatarajia ukarabati huu wa kivuko cha MV. KAZI utarudisha uhalisia wa ubora wa kivuko hicho kulinganana sheria za vyombo vya majini.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Songoro Mhandisi Khalid Songoro, akizungumza na mwandisi wa Habari wa TBC amesema ukarabati wa kivuko hicho kwa sasa umefikia asilimia 98. ‘’ Kivuko cha MV.KAZI kwa sasa kimeisha kwa asilimia 98 na kwa sasa tuko katika hatua za mwisho kabisa ili kukifanyia majaribio na kumalizia, lakini tunatarajia wiki ijayo tukishushe majini ili sasa kiweze kukaguliwa na mamlaka husika na baada ya hapo kuweza kurudi kutoa huduma,’’ amesema Mkurugenzi huyo.
Aidha Meneja pia ameeleza TEMESA ipo mbioni kukitoa kivuko cha MV. MAGOGONI kwenye maji mara tu baada ya kivuko cha MV.KAZI kurejea kutoa huduma ili nacho kiende kwenye matengenezo makubwa.
Mhandisi King’ombe alitumia pia wasaa huo kuwaomba radhi watumiaji wa vivuko vya Magogoni Kigamboni kutokana na kukosekana kwa huduma ya kivuko hicho kwa muda wote ambao kilikuwa kwenye matengenezo makubwa.