MAFUNZO MFUMO WA KIDIGITALI WA MUM YAENDELEA KUTOLEWA, SASA NI ZAMU YA DODOMA
Posted On: May 28, 2025
Mafunzo ya jinsi ya kutumia Mfumo wa Kidigitali wa Usimamizi wa kazi za Matengenezo MUM yameendelea kutolewa na wakufunzi wa mafunzo hayo na sasa ni zamu ya Mji Mkuu wa Kiserikali Dodoma. Mafunzo hayo ambayo yanatolewa kwa wadau wote wanaotumia huduma za TEMESA Nchi nzima, yalianza kutolewa mwanzoni mwa mwezi Machi mwaka huu na wataalamu kutoka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Mhandisi Pongeza Semakuwa ambaye ni Meneja wa Kikosi cha Umeme pamoja na Mhandisi Clement Abadyame, Meneja wa TEMESA Mkoa wa Mbeya.
Wakufunzi hao tayari wamezunguka katika Mikoa yote Nchini na wamebakiza Mkoa wa Dar es Salaam peke yake, mafunzo ya kutumia mfumo wa kidigitali wa MUM yanatolewa mahususi kwa ajili ya kuwafundisha watumiaji wa mfumo namna ya kuingia kwenye mfumo husika, kusajili magari ya Taasisi husika, majengo na vifaa vya umeme na elektroniki kwa ajili ya kuweza kuomba huduma za matengenezo kupitia mfumo huo tofauti na hapo awali ambapo mteja au Taasisi ili kupata huduma kutoka TEMESA ilihitajika kufika katika ofisi za TEMESA zilizo karibu ili kuweza kupata huduma hiyo.
Mafunzo ya jinsi ya kuutumia mfumo huo wa Kidigitali MUM, yanahusisha Maafisa Usafirishaji wa Taasisi za Umma, washitiri kutoka gereji teule ambao wanashirikiana katika kazi za matengenezo na TEMESA pamoja na watumishi wengine kama wahasibu na wagavi wa Taasisi za Umma ambao Taasisi zao zimewateua kwa ajili ya kuingia kwenye mfumo huo kuomba huduma za matengenezo ya magari pamoja na kazi zingine za Umeme na Elektroniki.
Mfumo huo wa Kidigitali wa Usimamizi wa Kazi za Matengenezo MUM, umebuniwa ili kurahisisha ufuatiliaji wa kazi za matengenezo, kuongeza uwajibikaji, na kuhakikisha huduma zinazotolewa na TEMESA zinaendana na viwango vya kitaifa na kimataifa na kupitia mfumo huu, ongezeko la ufanisi katika utendaji kazi na usimamizi wa mali za Umma ni jambo ambalo linatarajiwa kutokea.