MTENDAJI MKUU TEMESA ZIARANI MIKOA YA IRINGA, NJOMBE, MBEYA, RUKWA NA KATAVI

News Image

Posted On: March 13, 2019

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle ameendelea na ziara ya kutembelea mikoa mbalimbali kusikiliza changamoto pamoja na kukagua shughuli za utendaji kazi na safari hii ametembelea mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Rukwa na Katavi kukagua utendaji kazi wa karakana za mikoa hiyo.

Mhandisi Maselle alianzia ziara yake mkoani Iringa ambapo alipata fursa ya kuzungumza na wafanyakazi wa mkoa huo ambao walipata nafasi ya kumfikishia changamoto zao kubwa ikiwa ni upungufu wa wafanyakazi hasa mafundi wa karakana, mafundi wa viyoyozi pamoja na ukosefu wa vifaa vya kufanyia kazi za karakana ambapo waliomba kuongezewa nguvu kazi ili waweze kufanya kazi zao kwa urahisi zaidi kwani wanashindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha kutokana na upungufu huo.

‘’Katika mikoa yote niliyotembelea, upungufu wa wafanyakazi hasa wa karakana na vifaa kwa ajili ya mafundi wa karakana ndio tatizo kubwa tulilonalo wakala na nitahakikisha nalitafutia ufumbuzi’’, alisema Mhandisi Maselle. Aliongeza kuwa TEMESA haiwezi kupata mapato ya kutosha kufikia bajeti iliyojiwekea kama mapungufu haya yakiendelea kuwepo.

Aidha, Mhandisi Maselle alitembelea mkoani Njombe na kukutana na wafanyakazi wa mkoa huo ambako pia alipata pia fursa ya kukagua karakana ambapo alibaini mapungufu kadhaa ikiwemo uchakavu wa mitambo iliyopo katika karakana hiyo na kumuagiza Kaimu meneja kuhakikisha anaiondoa mitambo hiyo lakini pia ahakikishe anapunguza kupeleka kazi ndogondogo nje kwani kazi hizo ndizo zinazoongeza kipato kwa kiasi kikubwa hivyo kuzipeleka katika karakana teule ni kuwafaidisha wao.

Alimuagiza Kaimu meneja wa mkoa huo Mhandisi Saidi Mawazo kujenga tabia ya kushirikiana na mameneja wenzake wa mikoa mingine katika kujifunza mbinu mbadala za kuongeza mapato kwa kuweka utaratibu wa kutembeleana na kuona jinsi mkoa mmoja unavyofanya kazi zake na kuiga.

Mtendaji Mkuu alitembelea pia mkoa wa Mbeya na kukagua karakana ya mkoa huo na kuzungumza na wafanyakazi ambapo pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili ikiwemo upungufu wa akiba ya kutosha ya vipuri vya magari, vilainishi pamoja na madeni makubwa wanayodai baadhi ya taasisi mkoani hapo, Mhandisi Maselle aliahidi kuwaletea akiba ya kutosha ya vipuri hivyo mapema iwezekanavyo ambavyo tayari vimeshaagizwa kwa ajili ya karakana zote hapa nchini, aliwajulisha pia kuwa atatuma kamati yake ya madeni haraka iwezekanavyo ili kufuatilia mustakabali wa madeni hayo ambayo hayajalipwa muda mrefu na yanaendelea kuongezeka siku hadi siku.

Mara baada ya kutoka mkoani Mbeya, Mhandisi Maselle alitembelea mkoa waRukwa na kuzungumza na wafanyakazi wa mkoa huo akiwataka kuongeza juhudi kwani mkoa wao umekua haufanyi vizuri kimapato na kuwataka kujifunza kutoka kwa wenzao wa Iringa. Alimtaka meneja wa mkoa huo Mhandisi Fidoli Tumbi kujifunza mbinu mbadala za kuongeza mapato kutoka mkoa wa Iringa ambao kwa takwimu za hivi karibuni uekua ukifanya vizuri katika uzalishaji.

Mtendaji Mkuu alimalizia ziara yake mkoani Katavi ambapo alitembelea karakana ya mkoa huo na kuzungumza na wafanyakazi. Mtendaji Mkuu alibaini upungufu wa akiba ya vipuri vya magari, lakini pia alikuta chumba cha kuhifadhia vipuri kikiwa bado hakijakamilika na hivyo kumuagiza Meneja wa mkoa huo Mhandisi Stembrige Rushatila kuhakikisha anamalizia ujenzi wa chumba hiko na kukiwekea madirisha imara kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa vipuri hivyo. Mhandisi Maselle aliahidi kuwapelekea akiba ya vipuri na kuwataka kulitumia eneo kubwa walilonalo katika karakana hiyo kwa kuongeza huduma zingine ikiwemo uoshaji magari pamoja na kupaki magari nyakati za usiku kwa ajili ya kujiongezea kipato.