MTENDAJI MKUU TEMESA ATEMBELEA NA KUKAGUA KARAKANA MPYA IFAKARA

News Image

Posted On: June 11, 2019

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle ametembelea na kukagua karakana mpya ya TEMESA iliyopo katika Halmashauri ya mji wa Ifakara wilayani Kilombero mkoani Morogoro. Karakana hiyo ambayo imefunguliwa Juni mosi mwaka huu sasa itahudumia wilaya zote za karibu ikiwemo wilaya ya Ulanga na wilaya ya Malinyi ambazo awali zilikuwa zikitegemea kupata huduma za matengenezo ya magari na mitambo kutoka Morogoro mjini.

Akiwa kwenye karakana hiyo Mtendaji Mkuu alipata wasaa wa kuzungumza na wasimamizi wa karakana hiyo ambapo alipewa muhtasari wa kazi ambazo zimefanyika wakati wa kuanza kuikarabati karakana hiyo na Mhandisi Jairos Nkoroka ikiwemo usafi wa eneo la karakana hiyo kwa ujumla ikiwemo kurekebisha paa la karakana hiyo, kupaua, ujenzi wa choo kipya pamoja na uwekaji wa mifumo ya maji safi na maji taka pamoja na uwekaji wa mifumo mipya ya umeme ambao ulifanywa na ofisi ya TEMESA Morogoro.

Mhandisi Nkoroka pia alimueleza hatua mbalimbali walizozichukua ikiwemo kutembelea ofisi zote za serikali zinazopatikana katika wilaya ya Kilombero pamoja na wilaya za Ulanga na Malinyi ambapo waliweza kuzungumza na viongozi wa wilaya hizo kuanzia ngazi ya juu mpaka chini kuwakumbusha kuanza kupeleka magari yao, mitambo, pikipiki, kangavuke pamoja na kuleta kazi zote za elektroniki na umeme katika ofisi za wakala huo kama ambavyo sheria ya Manunuzi na Matengenezo ya magari inayvotamka.

Mhandisi Maselle aliwapongeza kwa kazi nzuri waliyoifanya mpaka kuwezesha kuanza kazi rasmi kwa karakana hiyo ambapo wameweza kusaidia kupungua kwa gharama za kufata huduma ya karakana ambazo mara nyingi zimekuwa zikitumiwa na baadhi ya taasisi za serikali kufata huduma hizo mjini Morogoro.

Awali Mhandisi Maselle alipata wasaa wa kukagua vifaa vya karakana hiyo vilivyonunuliwa mwanzoni mwa mwaka huu ambapo aliwaagiza kuvitunza na kuvitumia vizuri ili viweze kuwaletea mapato ya kuweza kujiendesha.

Aidha Mtendaji Mkuu alipata pia fursa ya kukagua kivuko cha MV Kilombero II pamoja na kivuko cha MV. Kilombero I ambavyo vimehifadhiwa katika karakana hiyo baada ya huduma za kivuko kufungwa katika mto Kilombero kutokana na kukamilika kwa daraja. Vivuko hivyo vinatarajiwa kuanza kufanyiwa ukarabati tayari kwa hatua ya kupelekwa katika eneo la Kikove Malinyi kwa ajili ya kutoa huduma katika maeneo hayo baadae mwaka huu.