MTENDAJI MKUU TEMESA ATEMBELEA MIKOA YA MANYARA, TABORA, KIGOMA NA RUFIJI PWANI

Posted On: March 13, 2019
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle ameendelea na ziara ya kutembelea mikoa mbalimbali kusikiliza changamoto pamoja na kukagua shughuli za utendaji kazi na safari hii ametembelea mikoa ya Manyara, Tabora, Kigoma na Pwani na kukagua utendaji kazi wa karakana za mikoa hiyo pamoja na kutembelea vivuko katika mikoa inayosimamia vivuko vya wakala huo.
Mhandisi Maselle alianzia ziara yake mkoani Pwani katika kivuko cha MV. MKONGO kujionea utendaji kazi wa kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba abiria 40 ambacho kinatoa huduma katika mto Rufiji kati ya Utete na Mkongo wilayani Rufiji mkoani Pwani.
Katika ziara hiyo, Mtendaji Mkuu aliambatana na Kikosi Kazi(Ferry Operation Safety Maintenance -FOSM)alichokiunda maalumu kwa ajili ya kuzungukia vivuko kote nchini, kubaini matatizo ya kiufundi ya vivuko hivyo na kuyatatua kwa wakati ili huduma za vivuko ziendelee kutolewa kwa ufanisi na kwa usalama. Kikosi Kazi hicho kikiongozwa na Fundi mkuu Reuben Matalu kilibaini matatizo kadhaa katika kivuko hicho na kuanza kuyafanyia kazi mara moja.
Vilevile, Mhandisi Maselle alipata nafasi ya kukagua eneo la maegesho ya kivuko ambalo awali lilikua likitumika kwa ajili ya kivuko cha MV. UTETE kupaki wakati wa kushusha na kupakia abiria ambalo limeharibika kwa kiasi kikubwa na aliahidi kulifkisha suala hilo kwenye menejimenti ya Wakala kwa ajili ya kulitafutia ufumbuzi.
Akiwa mkoani Manyara, Mtendaji mkuu alipata fursa ya kuzungumza na wafanyakazi wa mkoa huo ambao walipata nafasi ya kumfikishia changamoto zao kubwa ikiwa ni upungufu wa wafanyakazi hasa mafundi wa karakana, mafundi wa viyoyozi pamoja na ukosefu wa vifaa vya kufanyia kazi za karakana ambapo waliomba kuongezewa nguvu kazi ili waweze kufanya kazi zao kwa urahisi zaidi kwani wanashindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha kutokana na upungufu huo.
‘’Katika mikoa yote niliyotembelea, upungufu wa wafanyakazi hasa wa karakana na vifaa kwa ajili ya mafundi wa karakana ndio tatizo kubwa tulilonalo wakala na nitahakikisha nalitafutia ufumbuzi’’, alisema Mhandisi Maselle. Aliongeza kuwa TEMESA haiwezi kupata mapato ya kutosha kufikia bajeti iliyojiwekea kama mapungufu haya yakiendelea kuwepo.
Aidha, Mhandisi Maselle alitembelea mkoani Tabora na kukutana na wafanyakazi wa mkoa huo ambako pia alipata pia fursa ya kukagua karakana ambapo alibaini mapungufu kadhaa ikiwemo uchakavu wa mitambo iliyopo katika karakana hiyo na kumuagiza meneja kuhakikisha anaiondoa mitambo hiyo lakini pia ahakikishe anapunguza kupeleka kazi ndogondogo nje kwani kazi hizo ndizo zinazoongeza kipato kwa kiasi kikubwa hivyo kuzipeleka katika karakana teule ni kuwafaidisha wao.
Alimuagiza meneja wa mkoa huo Mhandisi Alfred Ng’hwani kujenga tabia ya kushirikiana na mameneja wenzake wa mikoa mingine katika kujifunza mbinu mbadala za kuongeza mapato kwa kuweka utaratibu wa kutembeleana na kuona jinsi mkoa mmoja unavyofanya kazi zake na kuiga.
Mtendaji Mkuu alimalizia ziara yake mkoani Kigoma ambapo alikagua kivuko cha MV. MALAGARASI chenye uwezo wa kubeba abiria 100 na magari 6 sawa sawa na tani 50 kinachotoa huduma katika Mto Malagarasi kati ya Ilagala na Kajeje mkoani humo.
Mara baada ya kumaliza kukagua kivuko hicho, alitembelea karakana ya mkoa huo na kuzungumza na wafanyakazi ambapo pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili ikiwemo upungufu wa akiba ya kutosha ya vipuri vya magari, vilainishi pamoja na madeni makubwa wanayodai baadhi ya taasisi mkoani hapo, Mhandisi Maselle aliahidi kuwaletea akiba ya kutosha ya vipuri hivyo mapema iwezekanavyo ambavyo tayari vimeshaagizwa kwa ajili ya karakana zote hapa nchini, aliwajulisha pia kuwa atatuma kamati yake ya madeni haraka iwezekanavyo ili kufuatilia mustakabali wa madeni hayo ambayo hayajalipwa muda mrefu na yanaendelea kuongezeka siku hadi siku.