MTENDAJI MKUU TEMESA APOKEA KIVUKO CHA MV ILEMELA-MWANZA
.png)
Posted On: April 19, 2020
Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) umepokea Kivuko cha MV Ilemela kilichotengenezwa kwa gharama ya Sh.bilioni 2.7 zilizotolewa na Serikali ya Tanzania.
Kivuko hicho kilitengenezwa na Kampuni ya kizalendo ya Songoro Marine Transport Boatyard ya jijini Mwanza ambapo kilianza kujengwa Aprili mwaka jana na kukamilika Februari 6, mwaka huu na kuingizwa majini kwa ajili ya kufanyiwa majaribio.
Akizungumza leo wakati wa mapokezi wa Kivuko hicho,Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Maselle alisema kwamba kivuko hicho kitaanza kazi rasmi ya kubeba abiria kutoka Kayenze kwenda kisiwa cha Bezi kwa gharama ya Shilingi 1000.
Mhandisi Maselle alisema kivuko hicho kina urefu wa mita 37, upana mita 10 na kitaelea ndani ya maji kati ya mita 0.75 hadi 1.4 ambapo kitakuwa na uwezo wa kubeba tani 100 zikihusisha abiria 200, magari 10 pamoja na mizigo.
“Kama mnavyoshuhudia Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya ghati la Kayenze sambamba na kisiwa cha Bezi ili Kivuko hiki kiweze kutia nanga vizuri, najua wakazi wa maeneo haya mmeteseka miaka mingi mkipata ajali na dhoruba nyingi lakini leo Serikali imewaletea usafiri wa uhakika’’.
“Nimeelezwa na wenyeji wa hapa kwamba mmekuwa mkilipa nauli ya Shilingi 3000 kwa kila mmoja lakini Serikali itawatoza kiasi cha Shilingi 1000 tu kutoka Bezi kwenda Kayenze, hivyo boti na mitumbwi iliyokuwa ikifanya kazi hapa, tumekubaliana ziende kubeba abiria wa visiwa vingine na kuwashusha Bezi ili kivuko hiki kiweze kuwaleta Kayenze,”alisema Mhandisi Maselle.
Mhandisi Maselle alisema kwamba licha ya kiviko hicho kuanza kazi lakini kitakuwa chini ya uangalizi wa TEMESA na mkandarasi Songoro kwa mwaka mmoja ambapo aliwataka wakazi wa eneo la Kayenze na Bezi kutumia fursa hiyo kuinua uchumi wao kwa kujenga nyumba za kisasa kama hoteli na masoko ya samaki.
Hata hivyo waliwataka wananchi kukitunza kivuko hicho kwa kuwa kimetengenezwa kwa fedha za watanzania wenyewe.
Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Dk. Angeline Mabula alimshukurua Mheshimiwa Rais Dk.John Pombe Magufuli kwa kukubali ombi lake la kujengewa kivuko ambacho alikiahidi kwa wananchi licha ya kutokuwapo katika ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mapokezi ya kivuko hicho yalihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela, John Wanga, Meya wa Ilemela, Renatus Muluga, viongozi waTEMESA makao makuu na mkoa wa Mwanza sambamba na wananchi wachache.