MTENDAJI MKUU TEMESA AFUNGUA MAFUNZO YA VIONGOZI TEMESA

Posted On: June 05, 2018
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Mgwatu ameutaka uongozi wa wakala huo kuongeza ufanisi katika utendaji wao wa kazi ili kupata matokeo bora na kuongeza tija katika wakala.
Dkt. Mussa Mgwatu ameyasema hayo leo wakati akifungua Mafunzo ya Uongozi kwa wakala huo yanayofanyika katika Ukumbi wa mikutano Bohari Kuu ya Madawa (MSD) Keko jijini Dar es Salaam yakiwa na lengo la kuwajengea uwezo wa kufanya maamuzi kimkakati na kwa wakati maalumu huku yakilenga zaidi masuala ya Akili Hisia, Uongozi Binafsi pamoja na kujitambua kama kiongozi.
‘’Furaha yangu kuhusu matayarisho ya siku ya leo yatakuwa ni mafunzo muhimu sana kwetu kwasababu naweza nikawa nikiwalaumu viongozi wangu kumbe siwawezeshi kufanya vizuri, nina uhakika mafunzo haya yatawawezesha kupata viongozi walio bora sio tu kwa TEMESA au Taifa bali viongozi wa Afrika na Dunia kwa ujumla’’, alisema Dkt. Mgwatu. Aliwahimiza pia viongozi wanaopatiwa mafunzo hayo kuyatumia vizuri ili kuhakikisha wanaporudi wanafanya kazi kwa bidii na kwa uaminifu mkubwa.
Naye mratibu wa mafunzo hayo kutoka Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute) Bi. Zuhura Sinare Muro aliwataka viongozi hao kuyazingatia mafunzo hayo na kuyapa kipaumbele kwani yatasaidia kuwaweka viongozi hao vizuri kimaadili na pia kuwaongezea tija na uzoefu katika utendaji wao. Bi Sinare aliushukuru pia uongozi wa TEMESA kwa kuwaamini na kukubali kupewa mafunzo hayo na Taaasisi hiyo.
Mafunzo hayo yatakayochukua siku nne yanatarajiwa kumalizika ifikapo ijumaa ya Tarehe 8 Mwezi wa Juni mwaka huu.