MTENDAJI MKUU TEMESA AFANYA ZIARA MIKOA YA ARUSHA NA KILIMANJARO

News Image

Posted On: March 13, 2019

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle amefanya ziara katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro na kuwataka wafanyakazi wa Wakala huo katika mikoa hiyo kuongeza juhudi katika kazi ili kuhakikisha wanazalisha kipato cha kutosha kuweza kufikia malengo au hata kuzidimapato waliyojiwekea kwa mwaka huu wa fedha wa 2018/2019.

Akizungumza na wafanyakazi hao kwa nyakati tofauti, Mhandisi Maselle alisema anatambua kwamba TEMESA inakumbwa na changamoto nyingi za kiutendaji ikiwemo ukosefu wa vifaa vya kutendea kazi hasa vya karakana pamoja na upungufu wa wafanyakazi lakini aliwataka mameneja wa mikoa hiyo pamoja na watumishi wake kujitahidi kufanya kazi zao kwa ufansi na kwa ushirikiano huku akiangalia namna ya kuwaongezea vitendea kazi na kujaza nafasi za watumishi zilizoachwa wazi baada ya kustaafu.

Katika mazungumzo yake Mhandisi Maselle alisisitiza kwamba, Kiongozi mzuri ni yule ambaye anafanya kazi bega kwa bega na wafanyakazi wenzake pale anapoona mapungufu na kuwatia moyo hivyo meneja ajitahidi kuwa karibu na watumishi wake.

Awali, Meneja wa TEMESA Mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Ferdinand Mishamo, alimpitisha Mtendaji Mkuu katika karakana ya mkoa ambapo alipata nafasi ya kukagua mashine na mitambo mbalimbali iliyopo katika karakana hiyo na baadae alimkaribisha katika kikao na watumishi na kumkumbushia kuhusu changamoto zinazoukumba wakala kubwa likiwa ni upungufu wa wafanyakazi ambapo karibu kila kitengo kina mtumishi mmoja mmoja ikiwemo kitengo cha uhasibu na kitengo cha manunuzi na kumuomba kuzifanyia kazi kwa wakati ili kuhakikisha watendaji wa mkoa huo wanapata wasaidizi ili waweze kutenda kazi zao kwa ufanisi. Mhandisi Maselle alimuahidi kumuongezea watumishi hasa katika upande wa karakana ambapo ndipo kuna upungufu mkubwa.

Katika hatua nyingine, akiwa mkoani Arusha, Mhandisi Maselle alipata pia wasaa wa kukagua mashine mbalimbali za kuchonga vipuri vya injini za magari, mashine za kuchomelea pamoja na mitambo mikubwa iliyopo katika karakana hiyo. Mtendaji Mkuu alimaliza ziara yake kwa kuzungumza na wafanyakazi wa mkoa huo na kuahidi kuzitafutia ufumbuzi kero zao kwa wakati ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi. Mhandisi Masellle alibanini kuwa matatizo ya karakana katika mikoa yote hiyo yanafanana na hivyo hayana budi kuchukuliwa hatua stahiki ili kuboresha utendaji wa karakana hizo.