MTENDAJI MKUU AITAKA TEMESA TANGA KUONGEZA UZALISHAJI
Posted On: March 13, 2019
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA Mhandisi Japhet Y. Maselle, amehitimisha ziara yake mkoani Tanga kwa kuwataka watendaji na viongozi wa Wakala mkoani humo kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa ili kuinua mapato ya kituo hicho.
Akizungumza na wafanyakazi wa TEMESA Tanga pamoja na mafundi wa karakana mara baada ya kuwasili mkoani humo, mhandisi Maselle aliwasisitizia suala la ubunifu hasa katika upande wa karakana ambapo aliwataka kuiga mfano kutoka mkoa wa Singida ambao uzalishaji wake umeongezeka kwa kipindi cha hivi karibuni kutokana na kubuni njia mbalimbali ili kuongeza pato lake ikiwemo kuepuka kupeleka kazi ndogo ndogo za ufundi katika karakana teule. Vilevile alipata pia fursa ya kusikiliza changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika utendaji kazi wao pamoja na kukagua baadhi ya mitambo iliyopo katika karakana hiyo. Changamoto kubwa iliyoonekana ilikuwa ni uchakavu wa mitambo ambapo Mhandisi Maselle alisema kuwa ni vyema sasa Wakala ukaanza utaratibu wa kununua mitambo mipya ili kuongeza ufanisi zaidi upande wa Ukodishaji mitambo.
Mhandisi Maselle pia alitembelea kivuko cha MV. TANGA ambacho kinatoa huduma ya kuvusha abiria kati ya Pangani na Bweni katika mto Pangani mkoani Tanga ambapo alikagua hali ya usalama wa kivuko hicho na kuendelea kusisitiza suala hilo kupewa kipaumbele kikubwa wakati wote wa uvushaji, ‘’hakikisheni mnatoa mafunzo ya usalama walau mara mbili kwa wiki maana wanaovuka hapa kila siku asilimia kubwa ni wakazi wa hapa hapa’’, alisema Mhandisi Maselle.
Aidha Mtendaji Mkuu, aliwapongeza kwa kuzingatia suala la nidhamu kwa viongozi wao lakini pia kusifia muonekano wa mabaharia wa kivuko hicho ambao walikua wamevalia sare zao zinazoweza kuwatambulisha kiurahisi kwa abiria na kuweza kupatiwa msaada pindi wanapohitaji.
Pamoja na kusikiliza kero, changamoto na maoni yao, Mtendaji Mkuu alipata pia wasaa wa kukagua kivuko cha MV. PANGANI II (kilichokuwa awali kinaitwa MV. UTETE kilichohamishwa kutoka Utete wilaya ya Rufiji mkoani Pwani) ambacho kinafanyiwa ukarabati mkubwa na Kampuni ya Kizalendo ya Songoro Marine Boatyard ya jijini Mwanza, kivuko hicho kinatarajiwa kuungana na kivuko cha MV. TANGA kutoa huduma eneo hilo mara tu ukarabati wake utakapokamilika.