MSONDE AITAKA TEMESA KUBORESHA NAMNA BORA YA UKUSANYAJI MAPATO
Posted On: September 20, 2024
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, ameutaka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania kuboresha mikakati ya ukusanyaji wa mapato kwenye vituo vyake Nchini ili kuongeza uwezo wa kifedha wa Wakala katika kufanikisha miradi zaidi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Dkt. Msonde, ameyasema hayo wakati alipofanya ziara ya kutembelea Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) mkoani Dar es Salaam hivi karibuni, kufuatia maagizo ya Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa ya kumtaka kufuatilia utendaji wa Wakala na kuhakikisha kuwa miradi inatekelezwa kwa viwango vya hali ya juu.
Katika ziara yake, Dkt. Msonde alitoa wito kwa TEMESA kutafuta mbinu mpya na za kisasa katika ukusanyaji wa mapato huku akisisitiza kuwa mifumo bora itasaidia kuimarisha huduma zinazotolewa kwa wateja, na Taasisi itaweza kujiridhisha na matumizi ya uendeshaji wa vivuko.
“Ni muhimu kuhakikisha kuwa kila shilingi inayokusanywa inatumika ipasavyo kwa ajili ya maendeleo ya wakala na wananchi, hii ni fursa nzuri kwa TEMESA kuonyesha ufanisi wake na kujenga uaminifu kwa wananchi. Tunatarajia kuona mabadiliko chanya katika ukusanyaji wa mapato na huduma zinazotolewa,” aliongeza.
Mathalani, akizungumza na viongozi na wahandisi wa TEMESA, Dkt. Msonde alisisitiza umuhimu wa utekelezaji mzuri wa kazi ili kukidhi mahitaji ya jamii ambapo alitoa wito kwa viongozi wa vituo vyote Nchini kujifunza kutokana na mbinu na mikakati inayotumika katika vituo ya Dar es Salaam, akisema kuwa ni fursa muhimu kwa maendeleo ya sekta ya ufundi na umeme.
“Nimeongea na baadhi ya madereva na Taasisi mbalimbali zinazohudumiwa na TEMESA hapa Dar es Salaam, hasa katika utengenezaji wa magari na Taasisi hizo zimeonyesha kuridhishwa na huduma zinazotolewa na TEMESA,” alisema Dkt. Msonde.
Aliongeza kuwa, “Huduma kwa wateja ni nzuri zaidi, ukaguzi wa magari unafanyika haraka. Ni muhimu kuwapongeza watendaji wetu, hasa katika Kanda hii ya Dar es Salaam, kwa kuboresha utendaji wao wa kazi na nitoe wito kwa mikoa yote Nchini kuiga utendaji bora wa TEMESA Dar es Salaam.”
Aidha, Dkt. Msonde ameipongeza TEMESA na kuitaka kutafuta ufumbuzi wa haraka kwa changamoto zinazoikabili, ambapo pia aliwaagiza watendaji wote kuzingatia ubora katika huduma ili kukidhi mahitaji ya wananchi na kuimarisha ufanisi wa shughuli zao.
Ziara hii ni sehemu ya juhudi za serikali katika kuhakikisha sekta ya ujenzi,uendeshaji na huduma za umeme zinaimarishwa kwa faida ya wananchi wote.