WAKAZI ZAIDI YA ELFU KUMI NA SABA TARAFA ZA NYAMIYAGA, RULENGE NGARA KUPATIWA HUDUMA YA KIVUKO
Posted On: July 25, 2025
Wakazi zaidi ya elfu kumi na saba wanaoishi eneo la Mayenzi kata ya Kibimba, Tarafa ya Nyamiyaga na Kanyinya, kata ya Mbuba, Tarafa ya Rulenge Wilayani Ngara Mkoani Kagera wanatarajia kuanza kupata huduma ya kivuko hivi karibuni baada ya Serikali kukamilisha ukarabati wa kivuko MV. OLD RUVUVU pamoja na miundombinu yake.
Huduma ya kivuko kwa Wakazi hao wa vijiji vya Mayenzi na Kanyinya ambao wanatenganishwa na Mto Ruvuvu imekua ya kuhatarisha maisha yao kwakuwa wamekuwa wakitegemea usafiri wa mitumbwi kutoka kijiji kimoja kwenda kingine hali ambayo imekuwa ikihatarisha usalama wao kutokana na kuwepo kwa viboko katika Mto Ruvuvu.
Mhandisi King’ombe amefika katika eneo hilo na amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wake wanaondokana na matumizi ya mitumbwi pamoja na kuwapa uhakika wa usafiri.
“Umesikia hapa mtumbwi huo mdogo unavusha watu na kuna viboko wanaweza wakapata madhara, lakini unapokuja na hatua kama hii ya kuleta kivuko unawaokoa wananchi na baadae Serikali yetu pendwa inapowafikia wananchi kwa kuwajengea miundombinu ya madaraja sisi vivuko tunaviondoa na kuvipeleka sehemu zingine.” Amesema Mhandisi King’ombe.
Katika ziara hiyo, Mhandisi King’ombe alipata wasaa wa kutembelea na kukagua utoaji wa huduma katika kivuko cha MV. RUVUVU kinachotoa huduma kati ya Rusumo na Nyakaziba Wilayani Ngara Mkoani Kagera.