MONGELLA AITAKA TEMESA KUCHANGAMKIA FURSA
Posted On: March 24, 2023
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella ameutaka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kuchangamkia fursa za matengenezo ya magari ya Serikali na binafsi Mkoani humo. Mhe Mongella ametoa kauli hiyo leo Tarehe 24 Machi, 2023 wakati alipohudhuria kikao cha wadau wanaotumia huduma za Wakala huo Mkoani Arusha kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Mhe. Mongella amesema anatamani kuona TEMESA inakua kimbilio la kwanza pale mtu anapotaka kutengeneza gari lake na ameongeza kusema kuwa soko la matengenezo ya magari ya Serikali ni soko kubwa sana na TEMESA ndio ambao wameundiwa soko hilo hivyo wanatakiwa kuchangamkia fursa hiyo.
‘’Pale mnapoacha fursa watatokea watu wataziba tu hilo pengo, na huo ndio utaratibu wa soko na si kwamba tunaposema TEMESA kwasababu ni Wakala wa Serikali maana yake watoa huduma wengine wafe, hapana, uwepo wao ndio ambao utaleta ufanisi kwenu vilevile. Kwahiyo mimi niombe TEMESA tuimarishe huduma na kwasababu Mtendaji Mkuu umeanzisha huu utaratibu wa kukutana na wadau wako mimi nafikiri hii ni hatua ya kwanza ya mafanikio.’’ Amesisitiza Mhe. Mongella na kuongeza kuwa ukishajua changamoto zako ukajua nani unaemlenga ukasema mkutane nae mjadiliane kwa uwazi maana yake wewe tayari umeshajua jambo la kufanya.
Mkuu wa Mkoa pia ametumia fursa ya kikao hicho kuwaomba wadau wote ambao kwa mujibu wa sheria na taratibu wanatakiwa kupata huduma za matengenezo ya magari, pikipiki na mitambo yao TEMESA, kuona ni kwa jinsi gani wanaweza kushirikiana na TEMESA na ameongeza kuwa ubora wa matengenezo ndio siri kubwa ya mafanikio ya Wakala huo.
Awali, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro N. Kilahala akizungumza katika kikao hicho cha wadau amesema Mkutano huo ni muendelezo wa mikutano ya aina hiyo ambayo TEMESA inaifanya nchi nzima ili kujisogeza karibu zaidi na wateja wake ili iweze kuelewa huduma inazowapa wanazipokeaje, maeneo ya changamoto ni yapi ili kwa pamoja waweze kujadiliana na kuyatafutia suluhu ya kudumu.
“Kwetu sisi hili ni zoezi endelevu na leo hii tupo hapa Arusha na tunashukuru kwa hii fursa ya kukutania hapa chini ya kivuli chako Mhe. Mkuu wa Mkoa. Hii inaonyesha TEMESA tuna mlezi hapa. Tunashukuru sana kwa hilo.’’ Amesema Mtendaji Mkuu.