WAZIRI ULEGA AIAGIZA TEMESA KUFANYA TATHMINI YA FAIDA ITAKAYOPATIKANA YA VIVUKO VIPYA VINAVYOJENGWA NA SERIKALI

News Image

Posted On: January 24, 2025

Waziri wa Ujenzi Mhe. Abdallah Ulega ameuelekeza Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kuhakikisha inafanya tathmini ya kujua ni nini athari chanya itapatikana kwa jamii kutokana na vivuko vipya sita vinavyoendelea kujengwa na Serikali kupitia Wakala huo katika maeneo mbalimbali hapa Nchini.

Waziri Ulega ametoa maagizo hayo leo Tarehe 24 Januari, 2025 wakati alipofanya ziara ya kiutendaji ya kukagua ujenzi wa vivuko vipya vinavyoendelea kujengwa na Serikali kupitia TEMESA eneo la Kanda ya Ziwa na Mkandarasi Songoro Marine katika Yadi yake iliyoko eneo la Pasiansi Wilayan Ilemela Mkoani Mwanza ambavyo vinagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 56 za Kitanzania.

Waziri Ulega amesema kuwa, uchumi wa Kanda ya Ziwa na uchumi wa Taifa la Tanzania unategemea sana miundombinu ya usafirishaji kwa hiyo, ujenzi wa vivuko hivyo vipya ni kitu muhimu sana kwa Taifa huku akiwataka TEMESA pamoja na Wizara ya Ujenzi kufanya tathmini ya athari zitakazotokana na ujenzi wa vivuko hivyo vipya.

“Mtoe tathmini ya kiuchumi na mtoe tahmini ya kijamii, ni kitu kizuri na ni kitu muhimu sana maana kinahusisha watu, maisha yao na ule mchango sasa wa kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na kwa Taifa ndo tunataka tuufahamu.”

Waziri Ulega pia amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha ambazo zimeweza kuwalipa wakandarasi akiwemo Mkandarasi Songoro Marine ili waweze kutekeleza miradi hiyo na kuikamilisha kwa wakati.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro Kilahala, amevitaja vivuko hivyo vipya vinavyoendelea kujengwa katika yadi ya Songoro ni kivuko cha MV. UKEREWE kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Kisorya Wilayani Bunda Mkoani Mara na Rugezi Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza ambako kinakwenda kukiongezea nguvu kivuko MV. UJENZI ambacho kimeonekana kuzidiwa na uwingi wa abiria wanaovuka kati ya maeneo hayo.

Aidha ametaja kivuko kipya cha MV. KOME III kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Nyakarilo na Kome Halmashauri ya Wilaya Buchosa, kivuko hicho pia kinakwenda kukiongezea nguvu kivuko MV. KOME ambacho kimeonekana kuwa kidogo kutoka na kuongezeka kwa abiria katika maeneo hayo.

Kivuko kingine kipya ni MV. BUKONDO kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Bwiro na Bukondo Wilayani Ukerewe Mkoani Mwanza, eneo hilo halijawahi kuwa na kivuko hapo awali na hivyo kivuko hicho kinakwenda kuchochea shughuli za kiuchumi na kibiashara katika maeneo hayo.

Vilevile amekitaja kivuko kipya kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Ijinga na Kahangala Wilayani Magu Mkoani Mwanza, eneo hilo pia halijawahi kuwa na kivuko na hivyo kinakwenda kuchochea hali ya kiuchumi eneo hilo.

Amekitaja pia kivuko kipya kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Buyagu Wilayani Sengerema na Mbalika Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza ambako pia hakukuwahi kuwa na kivuko hapo awali.

Kivuko kingine kipya cha sita ni kivuko kitakachokwenda kutoa huduma kati ya Mafia na Nyamisati Wilayani Mafia Mkoani Pwani ambacho kitakwenda kusaidiana na kivuko MV. KILINDONI ambacho kinatoa huduma katika eneo hilo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro Marine, Major Songoro, akizungumza katika ziara hiyo amesema kuwa kampuni ya Songoro inaendelea kufanya kazi usiku na mchana na itaanza kutoa vivuko vipya kuanzia mwezi Machi mwaka huu. ‎