WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI MHE. DKT. AKWILAPO AITAKA TEMESA KUENDELEA KUBORESHA UTOAJI HUDUMA

News Image

Posted On: July 05, 2026

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, leo tarehe 05 Julai 2026 ametembelea banda la Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza bandani hapo Mhe. Waziri Akwilapo ameitaka TEMESA kuendelea na maboresho katika kusimamia huduma za matengenezo ya magari pamoja na kuongeza umakini kwenye utoaji huduma sambamba na matumizi ya mifumo mipya ya kidigitali ili kuokoa muda.

‘’TEMESA mnapaswa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kujituma katika kutatua changamoto zinazowakabili wateja wenu. Nawapongeza kwa hatua mlizopiga katika matumizi ya teknolojia’’ amesema Dkt. Akwilapo. Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika matumizi ya mifumo ya kisasa ya kidijitali ili kurahisisha utoaji wa huduma, kupunguza muda wa kuhudumia wateja na kuongeza uwazi pamoja na uwajibikaji.

Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa taasisi za umma na sekta binafsi kuonesha bidhaa, huduma na ubunifu mbalimbali unaochochea maendeleo ya uchumi wa Taifa.