MAMENEJA TEMESA WAHIMIZWA KUBORESHA UTENDAJI KAZI WA KARAKANA
Posted On: May 24, 2019
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle amewataka mameneja wa Wakala huo wa mikoa yote nchini kuboresha utendaji kazi wa karakana za mikoa wanayoisimamia kwa kujifunza na kuiga uzoefu wa kazi miongoni mwao ili kuweza kupata ufumbuzi sahihi wa changamoto zinazowakabili katika karakana za mikoa yao.
Mhandisi Maselle ameyasema hayo mwishoni mwa wiki hii wakati akifungua kikao cha siku mbili kwa mameneja wa mikoa wa Wakala huo kuhusu utendaji kazi na namna ya kuboresha uendeshaji wa karakana za mikoa wanayoisimamia. Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha Ufundi VETA Iringa kilihudhuriwa pia na viongozi waandamizi wa Wakala huo wakiwemo wakurugenzi wa vitengo mbalimbali, mameneja wa vitengo na wakuu wa idara mbalimbali.
“Ni Imani yangu kuwa mapungufu yaliyobainika yatapatiwa suluhu katika kikao hiki kwani kimelenga kutoa mbinu kwa watendaji kupitia mawasilisho ambayo yatatolewa na wataalamu walioandaliwa na maelekezo mbalimbali yatakayotolewa na viongozi nilioambatana nao kutoka makao makuu’’, alisema Mhandisi Maselle.
Aidha Mhandisi Maselle aliongeza kuwa madhumuni ya kikao hiko ni kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa wakati wa mapitio ya utendaji kazi wa nusu mwaka wa mwaka wa fedha wa 2018/2019 katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Mt. Depot jijini Dar es Salaam ambapo katika kikao hicho ilibainika kuwa utendaji kazi wa vituo vya uzalishaji unatofautiana kutokana na kukosekana kwa uzoefu wa kazi, mbinu za kibiashara na usimamizi wa karakana kwa ujumla.
Vilevile Mhandisi Maselle alisisitiza kuwa kikao hicho kimefanyika mkoani Iringa kwasababu karakana ya mkoa huo ni kati ya karakana chache zinazofanya vizuri sana katika kutekeleza kazi zake kwa ubunifu mkubwa. Aliongeza, ''Naelewa kila mkoa una changamoto zake tofauti lakini huu ndio wakati sahihi wa kujadiliana kuhusu namna kila meneja anatatua changamoto zake hivyo tukijadili hapa inawezekana tukatoa ufumbuzi sahihi kwa wengine ambao huenda hawakuwa wakijua namna ya kutatua changamoto zinazowakabili na hilo ndilo jambo kuu ambalo tumekuja kujifunza hapa leo’’.
Naye mkuu wa chuo cha Ufundi VETA mkoa wa Iringa Ndg. Ng’wandu Luhende, awali alitoa mada kuhusu namna ya kupangilia na kuendesha karakana na namna ya kusimamia na kuendesha biashara kwa upande wa karakana ambapo alitoa wito kwa mameneja hao kuongeza tija katika uzalishaji ili kuviinua vituo vyao. Vilevile alimpongeza mtendaji mkuu kwa kuamua kuanza kupima utendaji kazi wa mameneja hao kila mwezi ili kuona tija ya kikao hicho na aliwaomba kutumia muda wao vizuri ili kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi wanaowasimamia katika vituo vyao.
Awali katika kikao hicho mameneja hao walimchagua Mhandisi Ian Makule, meneja wa TEMESA mkoa wa Iringa kuwa Mwenyekiti wa mameneja hao ambapo atahudumu kwa kipindi cha mwaka mmoja ambapo atakua akiendesha vikao vinavyofuata vya mameneja hao.