​WEZI WA MABOYA YA KUJIOKOLEA MAGOGONI KIGAMBONI WAPEWA ONYO

News Image

Posted On: March 10, 2024

Meneja wa vivuko Kanda ya Mashariki na Kusini Mhandisi Lukombe King’ombe ametoa onyo kwa (wezi) abiria wasio waaminifu wanaotumia kivuko MV. KIGAMBONI na MV. KAZI kuacha mara moja tabia ya uwizi wa maboya ya kujiokolea kwani wizi huo unasababisha kupungua kwa maboya hayo na hivyo kuhatarisha usalama wao pamoja na mali zao endapo itatokea dharura ya ajali wakati vivuko hivyo vinatoa huduma.

Mhandisi King’ombe ametoa onyo hilo leo Tarehe 10 Machi, 2024 wakati wa zoezi maalumu la kukagua na kuhesabu idadi ya vifaa vya kujiokolea vilivyomo ndani ya vivuko vinavyotoa huduma katika eneo hilo la Magogoni Kigamboni. Imegundulika kuwa, baadhi ya abiria wasio waaminifu, wamekuwa na tabia ya kuiba vifaa hivyo hasa maboya ya kujiokolea ya kuvaa (life jackets) ambayo ndiyo yanaonekana kuwa rahisi kubebeka bila kuonekana kwa urahisi wakati wa kushuka kutoka katika vivuko hivyo.

Wizi huo wa maboya ya kujiokolea umeonekana kushamiri na hata wakati mwingine kusababisha vivuko kusimamishwa kutoa huduma na Mamlaka husika za Usalama ikiwemo Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kutokana na kutokidhi vigezo vya usalama.

‘’Kwenye ukaguzi wetu tumekuta kuna upungufu mkubwa wa maboya ya kujiokoa na hili linatupa wasiwasi kwamba abiria wetu tunaowavusha baadhi wanachukua haya maboya, kwahiyo tunatoa onyo, tuna askari ambao wanazunguka na hivi vyombo lakini tuombe pia abiria wawe sehemu ya ulinzi wa vifaa hivi ambavyo vinatusaidia sote endapo itatokea dharura ya ajali.’’ Amesema Mhandisi King’ombe.

Sheria za usalama kwenye maji zinataka kivuko kuwa na maboya sawa na idadi ya abiria wote wanaobebwa na kivuko husika jumlisha asilimia kumi ya idadi ya abiria wanaobebwa na kivuko husika, mathalan kivuko MV. KAZI chenye uwezo wa kubeba abiria 800 kinapaswa kuwa na maboya zaidi ya 830 ili kukidhi matakwa hayo ya Kisheria, hivyo endapo kutakuwa na upungufu wowote wa maboya hayo, Mamlaka husika zinazo haki ya kusimamisha kivuko kisichokidhi kigezo hiko kutoa huduma mpaka kitimize sharti hilo ili kulinda uhai na mali za abiria wanaotumia kivuko husika endapo kitapata dharura ya ajali ambayo itahitaji abiria hao kuvalishwa maboya ya kujiokoa.

Mhandisi King’ombe ameongeza kuwa tabia hiyo ya wizi wa maboya ya kujiokolea imekuwa ikiingiza Serikali kwenye hasara kubwa kwakuwa inailazimisha itoe fedha nyingine mara kwa mara kwa ajili ya kugharamia ununuzi wa maboya mapya ili kukidhi matakwa ya kisheria ya uendeshaji wa vivuko pamoja na kuendelea kulinda uhai pamoja na usalama wa abiria na mali zao.

‘’Suala hili linapaswa kuacha kuendelea kujitokeza kwasababu Serikali inaingia gharama kubwa katika ununuzi wa vifaa hivi kwahiyo sote tunapaswa kuvilinda na kuheshimu kwamba vitatusaidia katika dharura endapo itajitokeza, kwahiyo narudia na kutoa rai na onyo kwa wale wenzetu ambao sio waaminifu ambao wanapunguza vifaa hivi vya kujiokolea katika vivuko vyetu.’’ Amesema Mhandisi King’ombe na kuongeza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika au kukamatwa akifanya matukio hayo ya uwizi wa maboya ya kujiokolea.

Vivuko MV. KAZI na MV. KIGAMBONI vinatoa huduma kwa masaa 24 katika eneo hilo na hivyo kutokana na sababu hiyo, vinapaswa kuwa na vifaa vya kujiokolea vya kutosha wakati wote vinavopokuwa vinatoa huduma kwa ajili ya kulinda usalama wa abiria wote wanaotumia huduma za vivuko hivyo ikiwemo majaketi ya kujiokolea, maboya ya kujiokolea, boti za uokozi, vizimia moto, vitambuzi moto pamoja na vifaa vingine mbalimbali vya kujiokoa endapo itatokea dharura ya ajali.