DKT. MSONDE AIPONGEZA TEMESA KWA KUSIMAMIA NA KUTEKELEZA MKAKATI WA MABADILIKO

News Image

Posted On: October 18, 2025

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, ameupongeza Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kwa juhudi thabiti na za dhati katika kusimamia na kutekeleza mabadiliko ya kiutendaji yanayoendelea ndani ya taasisi hiyo.

Akizungumza wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha Mameneja wa Mikoa, Wagavi na Wahasibu wa TEMESA kilichofanyika katika Hoteli ya Cate mkoani Morogoro, Dkt. Msonde alisema kuwa hatua zinazochukuliwa na TEMESA ni ishara ya uwajibikaji, dira na dhamira ya kweli ya uongozi wa taasisi hiyo katika kuijenga kuwa taasisi bora, yenye ufanisi na inayokidhi matarajio ya Serikali pamoja na wananchi.

“Nawapongeza viongozi wote wa TEMESA na watumishi tangu walipoanza maboresho haya ya utekelezaji wa mkakati huu tunao endelea nao mmefanya kazi kubwa na nawapongeza sana kwa kazi nzuri mliyoanza nayo kuifanya”, alisema Dkt. Msonde.

Alisisitiza kuwa mabadiliko ni jambo lisiloepukika katika taasisi yoyote inayotaka kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia na mazingira ya kazi, hususan katika maeneo ya magari na mifumo ya umeme.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Lazaro Kilahala, alisema kuwa kikao hicho kimekusudiwa kufanya tathmini ya mapato na matumizi ya taasisi, huku kikilenga pia kupokea mrejesho wa utekelezaji wa mkakati wa mabadiliko unaoendelea.

“Kupitia kikao hiki, tunajadiliana kwa kina kuhusu namna tunavyoweza kutekeleza kwa mafanikio mkakati wa kuijenga TEMESA imara, isiyoingia kwenye madeni, na yenye kutoa huduma bora kwa wateja wake,” alisema Kilahala.