WAKUU WA WILAYA LINDI MTWARA WAZITAKA TAASISI KULIPA MADENI WANAYODAIWA NA TEMESA
Posted On: June 27, 2023
Wakuu wa Wilaya za Lindi na Mtwara wameziagiza Taasisi zilizoko Mikoani humo kuhakikisha wanalipia gharama za huduma wanazopatiwa na Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) ili kuuwezesha Wakala huo kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Wakuu hao wa Wilaya, wameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati wa vikao vya wadau vilivyoandaliwa na TEMESA na kufanyika katika Wilaya zao kwa lengo la kuendelea kupeana mrejesho baina ya TEMESA na wadau wake kwa ujumla ambao ni wauzaji wa vipuri, watengenezaji wa vilainishi, Taasisi za Umma na Serikali pamoja na watu binafsi ikiwa ni muendelezo wa jitihada za Wakala huo katika kuboresha utendaji kazi wake ili kuhakikisha wateja hao na Serikali wanawezeshwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi bila vikwazo vyovyote.
Akizungumza wakati wa Kikao cha wadau Mkoani Lindi, kilichofanyika katika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo Tarehe 22 Juni, 2023, Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga amewaomba wadau hao kuendelea kupata huduma TEMESA huku akiwataka kuhakikisha wanalipia gharama za huduma baada ya kumaliza kutengenezewa magari yao na mitambo
''Lakini tukipata huduma tulipe, Mheshimiwa Rais hawezi kuhudumia tu kila siku, hapana, itafika mahala Taasisi lazima ijiendeshe angalau kwa asilimia fulani, sasa hawawezi kuwa wanaenda kuchukua vipuri huko wakufungie halafu hulipi, wanakuja kukurekebishia wewe hulipi,wataishi vipi, na hawa tumewapa uwezo wa kufanya shughuli zao kutegemea na malipo ambayo wanayapata, kwahiyo tukalipe.'' amesisitiza Ndemanga na kuwataka TEMESA kuhakikisha wanakagua madeni hayo vizuri ili kuona namna yanavyoweza kulipika, amewaomba pia kutokataa kutengeneza magari ya Taasisi ambazo zinadaiwa.
Mkuu huyo wa Wilaya pia ameipongeza TEMESA kwa maboresho ambayo inaendelea kuyafanya katika karakana zake na kuziomba Taasisi za Umma na wadau kuiamini TEMESA kwakuwa imebadilika na inafanya kazi kwa ufanisi mkubwa. ''TEMESA sasa imeboreka, kwa wale ambao tumepata nafasi ya kukagua na kusikiliza kule nje, sio TEMESA ile ambayo tulikuwa nayo miaka iliyopita, kwahiyo niwaombe tuondoe hofu, twendeni tupeleke magari yetu TEMESA, twendeni tuwaite maofisini kwetu warekebishe wakague viyoyozi, waje kwenye nyumba zetu waangalie pia umeme, wana vifaa vya kisasa vya kukagua na kutengeneza viyoyozi vyetu, wana vifaa vya kisasa vya kupima umeme kwenye nyumba zetu, twendeni tuwatumie TEMESA.'' Amesema Ndemanga na kuongeza kuwa Wakala huo kwa sasa umebadilika na gharama zake sasa zinaendana na soko tofauti na zamani huku akiwahakikishia wadau wa Mkoa wa Lindi ubora wa huduma kutoka Wakala huo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Hanafi Msabaha, akizungumza na wadau hao Mkoani humo mwishoni mwa wiki, amewataka wadau hao kutokata tamaa na TEMESA, kurejesha imani yao kwa TEMESA na kuendelea kufanya kazi nao na kama itajitokeza changamoto basi wadau hao wasisite kuileta mbele yake ili izungumzwe na kutatuliwa. Msabaha amesema vikao vya aina hiyo viwe endelevu kwa TEMESA kuendelea kukaa na wadau wake na kutathmini namna wadau hao wanavozitafsiri huduma za Wakala, wapi wanakosea na wapi wapaboreshe zaidi ili TEMESA iendelee kutoa huduma bora. Msabaha pia amesisitiza suala la wadau hao hasa Taasisi za Umma kulipa madeni yao kwa wakati.
''Lakini ndugu wadau, tunapopata huduma za TEMESA basi mimi niwaombe na sisi tuwe waaminifu tulipe mapema, na mara nyingi Taasisi za Serikali na Wakala za Serikali zinazotoa huduma zinakwama kwasababu hiyo, Taasisi ni za kwetu wenyewe lakini tunakopa hatulipi, lakini mjue kwamba kuwa na madeni mengi pia inasababisha Taasisi kushindwa kujiendesha.'' Alimaliza Msabaha.
Aidha, Mtendaji Mkuu wa Wakala huo, Lazaro N. Kilahala, akizungumza kwa nyakati tofauti katika vikao hivyo, amesema TEMESA imekuwa ikifanya vikao na wadau kwa ajili ya kuendelea kupeana mrejesho ikiwa ni muendelezo wa jitihada za kuboresha utendaji kazi wa Wakala huo ili kuwezesha wateja na Serikali kwa ujumla kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi bila vikwazo vyovyote. Kilahala amesema vikao hivyo ni muendelezo kwani TEMESA iko katika kufanya mabadiliko makubwa na lazima iwashirikishe wadau wake katika kujua maeneo gani izidi kuyaboresha lakini pia kupeana mrejesho kwa maeneo ambayo tayari Wakala huo umekwishaanza kuyafanyia kazi.
Kilahala ametoa shukrani za dhati kwa Mhe. Rasi Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Awamu ya Sita kwa ujumla kwa uwekezaji mkubwa ambao inaendeleea kuufanya TEMESA, amesema kuwa Serikali imekuwa ikiendelea kununua vitendea kazi kila mara na vimekuwa vikisambazwa kila Mkoa kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi wa Wakala huo. ''Karakana zetu zinaendelea kufanyiwa ukarabati mkubwa na watumishi wetu wanaendelea kupatiwa mafunzo, hii yote ni katika kuboresha huduma na utendaji wa Wakala, hatuna sababu ya kurudi nyuma, uwekezaji huu unaofanyika na dhamira ya dhati ya Serikali yetu ni kuona kwamba TEMESA inakuwa bora zaidi na inakuwa inachangia pakubwa zaidi katika maendeleo ya nchi yetu, kwahiyo hatuwezi kurudi nyuma.'' Amesema Kilahala na kuongeza kuwa anawakaribisha wateja katika TEMESA mpya, ambayo inafanya kazi kisasa, kwa vifaa vya kisasa, vitendea kazi vya kisasa, TEMESA ambayo inataka kubadilika na kuishi matarajio ya wateja wake, sio TEMESA kwa mujibu wa Sheria bali TEMESA inayotaka kumridhisha mteja ili aweza kufurahia huduma anayoipata.
Kilahala alimaliza kwa kutoa wito kwa Taasisi za Umma na wadau waendelee kuiamini TEMESA na kuendelea kufanya kazi na TEMESA na kuongeza kuwa Wakala unakuja kivingine kuhakikisha wateja wanaridhishwa huku akiwasihi wadau hao kulipa mkazo suala la ulipaji wa madeni ya huduma wanazopatiwa kwani wakilipa madeni yao, TEMESA itaweza kulipa wazabuni kwa vipuri ambayo inawauzia ili wateja hao waridhishwe na huduma wanazopatiwa.