LUTENI KANALI MALECELA AVUTIWA NA TEKNOLOJIA YA TEMESA KATIKA MAONESHO YA NANENANE

News Image

Posted On: August 05, 2025

Kamanda wa Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Luteni Kanali Nyagalu Malecela, ametembelea banda la Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) katika maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nanenane) yanayofanyika katika Viwanja vya Ngongo, mkoani Lindi.

Akiwa ameambatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Bi. Azilongwa Bohari, pamoja na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Sheria Mkoa wa Lindi, Adv. Mariam Kashule, Kamanda Malecela alipata maelezo ya kina kutoka kwa maafisa wa TEMESA kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo.

Katika ziara hiyo, viongozi hao walielimishwa kuhusu Mfumo wa Usimamizi wa Kazi za Matengenezo (MUM) unaotumiwa na TEMESA kusimamia kwa ufanisi shughuli za matengenezo ya magari na hudumba mbalimbali zitolewazo na TEMESA.

Pia walipatiwa elimu juu ya matumizi ya vifaa vya kisasa vya ukaguzi wa vyombo vya moto, vinavyosaidia kuhakikisha magari na mitambo inayoingia kazini inakuwa katika hali bora na salama kwa matumizi ya serikali.

Aidha, TEMESA iliwaonesha vifaa vya uokozi majini na kueleza namna wanavyotumia teknolojia ya kisasa kuhakikisha usalama katika vivuko na huduma za usafiri wa majini.

TEMESA Lindi inawakaribisha wananchi wote kuendelea kutembelea banda lao ili kupata elimu na huduma mbalimbali zitolewazo, kwa maendeleo ya taifa letu.