‘’TUANZE KUZIFANYIA KAZI CHANGAMOTO’’ MTENDAJI MKUU TEMESA

News Image

Posted On: December 21, 2021

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Lazaro N. Kilahala leo amefanya ziara fupi ya kiutendaji na kuwaagiza watumishi wa Mkoa wa Dodoma kuanza kuyafanyia kazi malalamiko ya wateja wanaohudumiwa na karakana hiyo. Akiwa katika ziara hiyo fupi, Mtendaji Mkuu alianza kwa kutembelea karakana ya TEMESA Mkoa wa Dodoma, ametembelea pia eneo la ujenzi wa karakana mpya ya mfano inayojengwa eneo la Kizota pamoja na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya la Makao Makuu ya Wakala huo linalojengwa katika eneo la NCC mtaa wa Tambukareli mjini Dodoma.
Akizungumza na menejimenti ya karakana ya TEMESA mkoa wa Dodoma inayoongozwa na meneja wa TEMESA Mkoa wa Dodoma Mhandisi Julius Humbe, Mtendaji Mkuu amesema ni wakati sasa Wakala unatakiwa kuona kuwa mahusiano mazuri na wateja wetu ni jambo la kipaumbele hivyo kuweka utaratibu wa kupokea na kufanyia kazi maoni ya wateja huku tukijikita kutatua kero zinazoripotiwa kwa wakati.

‘’Tunafanya hivi kwasababu ya kujenga uhusiano mzuri na wateja wetu, hawawezi wakawa wanalalamika kila siku halafu hawaoni sisi tunafanya nini, huduma zetu zisipokuwa bora tunajifunga sisi wenyewe’’.
Awali, meneja wa TEMESA Mkoa wa Dodoma Julius alieleza changamoto wanazokumbana nazo katika utendaji wao wa kila siku ambapo alizitaja baadhi ya changamoto kuwa ni upungufu wa watumishi, changamoto ya upatikanaji wa vipuri, na kucheleweshwa malipo kwa kazi zilizofanywa.
Akijibu baadhi ya changamoto hizo, Mtendaji Mkuu, ameieleza menejimenti ya mkoa kuwa kwasasa upo mpango mkakati wa kuboresha utendaji wa TEMESA unaojumuisha mapendekezo ya namna kero hizo tatu zitakavyotatuliwa. Hivyo watajulishwa pale maamuzi yatakapofanywa juu ya mpango huo. Kwa sasa tujikite kuzifahamu na kutatua kero za wateja wetu maana hilo liko ndani ya uwezo wetu wakati huu.
‘’Tusichukie, tuwe tayari kukosolewa na tufanyie kazi ili kujenga imani kwa wateja wetu.'' Alimaliza Mtendaji Mkuu na kuongeza kuwa wateja wakituamini tufanikiwa na wasipotuamini hatutafanikiwa.

Tanzania Census 2022