​‘’TUENDELEE KUIUNGA MKONO SERIKALI YETU KWASABABU NI SERIKALI SIKIVU NA INATATUA KERO ZA WANANCHI,’’ MTENDAJI MKUU TEMESA

News Image

Posted On: December 14, 2024

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro Kilahala amewaomba wananchi wa Kanda ya Ziwa na maeneo mengine ya Nchi kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita inayooongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwakuwa Serikali hiyo ni Serikali sikivu inayowajali wananchi wake kwa kutatua kero zinazowakabili hasa za usafiri wa maji ambao ndio umekuwa tegemeo kubwa kwa wakazi wanaoishi visiwani na pembezoni mwa Ziwa Victoria.

Kilahala ameyasema hayo leo Tarehe 15 Desemba, 2024 wakati alipofanya ziara ya kikazi katika eneo la Buyagu Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza, kukagua maendeleo ya ujenzi wa maegesho mapya ya kivuko cha Buyagu- Mbalika yanayoendelea kujengwa katika eneo hilo.

Kilahala amesema, katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa, Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inafanya kazi ya ujenzi wa vivuko vipya vitano huku vitatu kati ya hivyo vikiwa vinatarajiwa kupelekwa katika maeneo ambayo hayakuwahi kabisa kuwa na vivuko hapo awali na viwili vinapelekwa maeneo ambayo vivuko vilikuwepo lakini mahitaji yameongezeka na hivyo kuhitaji vivuko vikubwa zaidi ili kuhakikisha wananchi hao wanapata huduma nzuri na ya kuridhisha.

‘’Hapa tuko eneo linaitwa Buyagu, kuna kivuko kipya kitakuja hapa kitakuwa kinafanya kazi kati ya hapa Buyagu na upande wa pili unaitwa Mbalika, lakini katika vile vivuko vitatu vipya nilivyovisema kingine kitapelekwa Ijinga- Kahangala ambako pia ni eneo ambalo lilikuwa halina huduma ya kivuko kabisa na kivuko kingine cha tatu kitapelekwa Bwiro- Bukondo, haya ni maeneo yalikuwa hayana vivuko.’’ Amesema Kilahala.

Mtendaji Mkuu ameongeza kuwa, baada ya kukamilisha ujenzi wa maegesho katika vituo, Serikali itaendelea na ujenzi wa majengo ya kupumzikia abiria (Waiting Lounges) wakati wakisubiri vivuko na amesema uwekezaji huo wa ujenzi wa maegesho ya vivuko pamoja na ujenzi wa majengo ya kupumzikia abiria (Waiting Lounges) utaendelea pia kufanyika katika maeneo yote mapya ikiwemo Ijinga-Kahangala na Bwiro-Bukondo. Aidha amesema kuwa maeneo ya Kisorya na Rugezi pia, uendelezaji wa miundombinu unafanyika ambapo majengo ya kupumzikia abiria na maegesho mapya yenye viwango vya kisasa, yanaendelea kujengwa na Serikali ili kuboresha utoaji huduma.

‘’Kipekee kabisa tunaipongeza na kuishukuru Serikali yetu kwasababu ni Serikali sikivu inaangalia mahitaji na shida za wananchi na kuzipatia majibu, mfano hapa Buyagu-Mbalika, wananchi wamekuwa na shida ya usafiri kwa zaidi ya miaka ishirini hawakuweza kupata kivuko, lakini Mheshimiwa Rais ndani ya miaka yake mitatu hii tunaona nini kinaendelea nyuma yetu, ni Serikali sikivu, Serikali inayotatua changamoto na madhila yanayowakabili wananchi ili kuhakikisha maisha ya wananchi yanaendelea kuwa bora.’’ Alisema Kilahala na kuongeza kuwa hayo ndiyo maono ya Mheshimiwa Rais ya kutaka kuona wananchi wake wanaishi na kupata huduma katika ubora ambao ni stahiki.

Naye Mkandarasi anayesimamia ujenzi wa maegesho hayo kutoka Vikosi vya ujenzi, QS Basesa Nyendeza Simion, amesema ujenzi wa maegesho ya kivuko upande wa Buyagu tayari umefikia asilimi sitini na mara watakapomaliza kazi hiyo upande wa Buyagu watahamia upande wa Mbalika. Basesa ameongeza kuwa maegesho mengine wanayoyasimamia ni yale yaliyoko Mkoa wa Mara eneo la Mwigobero ambayo ujenzi wake unaendelea na umefikia asilimia saba pamoja na maegesho ya Bukimwi upande wa Wilaya ya Ukerewe ambako ujenzi wake umefikia asilimia sabini. Basesa ameongeza kuwa maegesho yote hayo ujenzi wake unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi wa sita mwaka 2025.

Katika ziara hiyo, Kilahala ameambatana na Mkurugenzi wa Uendeshaji na Ujenzi wa Vivuko Mha. Sylvester Simfukwe ambapo ziara yao ilianzia katika eneo la Ilunda- Luchelele ambako walikagua maendeleo ya ujenzi wa maegesho unaoendelea katika kituo hicho kabla ya kwenda Wilaya ya Magu ambako nako pia walipata fursa ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa maegesho mapya ambapo kwa upande wa Kahangala maegesho hayo yamefikia hatua za mwisho za ujenzi wake, walifika pia upande wa Ijinga ambako kazi ya usombaji wa mawe ya kujengea maegesho hayo inatarajiwa kuanza hivi karibuni, wamekagua pia maegesho ya Mwigobero-Kinesi Wilayani Musoma pamoja na Kisorya Wilayani bunda kabla ya kumaliza ziara yao leo katika eneo la Buyagu Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza.