KWANDIKWA AAGIZA BILIONI 32 ZILIPWE TEMESA

News Image

Posted On: October 28, 2019

Naibu Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Elias Kwandikwa ameziagiza taasisi zote za serikali zinazodaiwa madeni na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) yanayofikia jumla ya shilingi bilioni 32 kuhakikisha zinalipa madeni hayo haraka iwezekanavyo ili kuusaidia Wakala huo kutimiza majukumu yake.

Mhandisi Kwandikwa ametoa maagizo hayo leo wakati akikagua vitendea kazi vipya vilivyonunuliwa na TEMESA kwa ajili ya kuvisambaza kwenye karakana zake.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kwandikwa alisema anaelewa changamoto zinazoukabili Wakala ikiwemo kutolipwa madeni kwa wakati ambapo alisema Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2019/20 imetoa fedha zote zilizokuwa kwenye bajeti zinazohusu karakana ili TEMESA ikamilishe ukarabati wa karakana na ununuzi wa vitendea kazi ambapo alielekeza miradi yote iliyokuwa imepangwa na imepelekewa fedha, utekelezaji wake ukamilike kwa wakati.

‘’Ninaelekeza Taasisi zote za Serikali zilipe madeni zinazodaiwa na TEMESA kiasi cha Shilingi bilioni 32’’. Aliongeza Naibu waziri.

Awali Naibu waziri alipata wasaa wa kukagua vitendea kazi hivyo vipya vya karakana pamoja na karakana mbili mpya zinazotembea (Mobile Workshop Track) kwa ajili ya matengenezo ya magari yaliyo mbali na karakana za mikoa na magari yaliyopata hitilafu yakiwa safarini.

Aidha alitoa wito kwa watumishi wa Wakala kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha magari yanafungwa vipuri halisia na hivyo kuondoa malalamiko yaliyozoeleka kuwa magari yakitoka katika karakana za TEMESA huharibika baada ya muda mfupi.

‘’Ninaagiza kudhibiti gharama za matengenezo ambazo nazo hulalamikiwa. Mnapaswa kununua vifaa (vipuri) kwa pamoja (Bulk procurement) ili kupata punguzo la bei’’.

Naye Mtendaji Mkuu wa TEMESA Mhandisi Japhet Maselle, akisoma taarifa fupi katika hafla hiyo, alisema Vitendea kazi hivyo vimegharimu jumla ya shilingi milioni 260 na vitasambazwa katika vituo 12 ikiwemo karakana ya Dodoma, Ruvuma, Geita, Kigoma, Rukwa, Pwani, Shinyanga, Katavi, Mwanza, Songwe, Same na Kahama. Vilevile, gari itakayotumika kama karakana ya dharura pamoja na vitendea kazi vyake imegharimu jumla ya shilingi milioni 115 na gari hiyo itafanya kazi sambamba na magari madogo mawili

‘’Tutafanya ununuzi wa vitendea kazi kwa ajili ya karakana zingine 14 pamoja na hayo tunaishukuru serikali kwani tumepokea shilingi bilioni 12.4 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya karakana pamoja na vivuko, nakuahidi fedha hizi zitatumika kama zilivyokusudiwa na kwa ufanisi mkubwa’’, alisema Mhandisi Maselle.

Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA una jumla ya karakana 26 katika makao makuu ya mikoa kote nchini pamoja na karakana moja ngazi ya wilaya katika mji wa Ifakara katika wilaya ya Kilombero.