KILAHALA AENDELEA NA ZIARA, LEO NI SIMIYU & SHINYANGA
Posted On: October 20, 2022
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania Lazaro N. Kilahala leo ameendelea na ziara yake ya kiutendaji ambapo amemtembelea Mkuu wa Mkoa wa Simiyu pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ili kupata mrejesho, maoni na changamoto wanazokutana nazo, namna wanavyopokea huduma wanazopatiwa na ofisi za Wakala huo katika Mikoa yao na nini wanatamani kiboreshwe ili kuimarisha huduma za TEMESA katika Mikoa husika.
Mtendaji Mkuu alianza ziara yake Mkoani Simiyu ambapo amekutana na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Yahaya Nawanda ambaye aliipongeza ofisi ya TEMESA Mkoa na kuwaahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha katika kutimiza majukumu yao ikiwemo kuwalipa madeni yote ambayo Wakala unazidai Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ambapo jumla ya deni linalodaiwa linafikia kiasi cha shilingi milioni 530.
‘’Tutapunguza madeni kwasababu tusipofanya hivyo TEMESA hamuwezi kujiendesha, tukipata huduma basi na sisi tunapunguza angalau hata milioni moja au mbili kila mwezi ili na nyie mjiendeshe pia na muweze kuendelea kutoa huduma bora na sisi tuendelee kupata huduma’’. Alisema Mhe Nawanda na kumuagiza Meneja wa TEMESA Mkoa wa Simiyu Mhandisi Julius Humbe kuandaa kikao cha pamoja kati ya TEMESA na wakurugenzi wa taasisi zote za Mkoa wa Simiyu ili waweze kujadili kuhusu madeni yao na namna ya kuyalipa.
Mhe. Nawanda pia alimuagiza Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo kuhakikisha kila mwisho wa mwezi anapoandaa malipo awe anawasilisha katika orodha ya mgao kiasi cha deni kuilipa TEMESA ili kupunguza deni wanalodaiwa na Wakala huo.
Akiwa mkoani Shinyanga, Mtendaji Mkuu amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Sophia Mjema ambaye ameushauri Wakala kuwa na utaratibu wa kuwapeleka mafundi wake kwenye mafunzo ili kuendana na kasi ya teknolojia mpya za magari ambazo zinabadilika kila uchwao, kuhakikisha wanakua na vipuri vya kutosha vyenye ubora katika karakana wakati wote, kujaribu kuweka ubia na wauzaji wa vipuri na ikiwezekana wawepo ndani ya karakana ili kuokoa muda pamoja na kupunguza muda wa matengenezo ya magari.
‘’ Haya ndio mambo ambayo watu wengi wanalalamikia, hivyo ni wajibu wenu TEMESA kuhakikisha mnayafanyia kazi, TEMESA ni Taasisi yetu tumeianzisha, tunataka iendelee kutoa huduma bora, tunategemea makubwa kutoka kwenu” alimaliza Mheshimiwa Sophia Mjema.
Kwa nyakati tofauti, Mtendaji mkuu Aliwashukuru wakuu hao wa Mikoa kwa mawazo, ushauri na nasaha walizotoa huku akisisitiza ni muhimu kubadilika na aliahidi TEMESA itajitahidi kujiimarisha na kuyafanyia kazi mawazo yote waliyowapatia ili hiyo iwe ndio taswira ya TEMESA na hata itakavyoendelea ili yale ambayo inapaswa kuyafanyia kazi yaendelee kuboreshwa.