KILAHALA NA TIMU YAKE WAZURU MTWARA
Posted On: November 09, 2022
Lazaro Kilahala, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) pamoja na timu yake, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi (DBSS) Bi. Josephine Matiro pamoja na Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi (DMTS) Mhandisi. Hassan Karonda, leo wameendelea na ziara ya kiutendaji Mkoani Mtwara ambapo wametembelea karakana ya Mkoa huo na kuzungumza na watumishi, wamekagua utendaji kazi wa kivuko cha MV. MAFANIKIO kinachotoa huduma kati ya Msangamkuu na Msemo Mtwara Mjini kabla ya kuhitimisha ziara yao katika kivuko cha MV. KILAMBO kilichokuwa kinatoa huduma kati ya Kilambo Mtwara na Namoto Msumbiji. Kivuko hicho kimesimama kutoa huduma kwa muda mrefu kutokana na kukauka mara kwa mara kwa Mto Ruvuma na kusababisha kivuko kisimame kutoa huduma na kwa mujibu wa Kilahala, kivuko hicho kitafanyiwa ukarabati mkubwa na kuhamishwa kwenda kutoa huduma eneo jingine lenye uhitaji.
Mapema asubuhi Kilahala alizungumza na watumishi wa karakana ya Mkoa huo na hapa namnukuu akiwakumbusha kuhusu miongozo ya utendaji kazi (Performance Agreements) ambayo kila mtumishi ataingia makubaliano hayo ya kiutendaji na kiongozi wake wa kazi na kutakiwa kuzalisha kile alichokubaliana na kiongozi wake inapofikia mwisho wa mwaka;
''Maana kubwa ya makubaliano haya ni kwa kila siku, kila mmoja wetu atambue anatakiwa kufanya nini ili aweze kufikia malengo ya Taasisi na miongozo ya utendaji kazi isiwe tu karatasi, niwaombe tuipitie mara kwa mara na kuhakikisha mienendo yetu inapitia kwenye miongozo ile.''
''Uwazi, umoja, ushirikiano ni nguzo kubwa kwa maendeleo ya Taasisi yoyote ile duniani,shirikianeni ili muweze kufanikiwa pamoja na sio vibaya mkiiga kwa wenzenu wa Mikoa mingine, mimi naomba kuanzia leo tubadilike, tupendane, tuwe wamoja na tushirikiane kuipeleka TEMESA mbele.'' Josephine Matiro, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi TEMESA akizungumza na watumishi wa TEMESA Mtwara.
''Serikali inatoa vitendea kazi vya karakana kila mwaka, ni jukumu lenu kuvitunza vitendea kazi hivyo ili vitusaidie katika utendaji kazi wetu, lengo letu nikufikia malengo ya Taasisi na kuboresha maisha yetu.'' Eng. Hassan Karonda, Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi TEMESA akizungumza na watumishi wa TEMESA Mtwara leo.