KILAHALA ASISITIZA UWAJIBIKAJI NA UJITEGEMEZI WA VITUO VYA TEMESA
Posted On: June 17, 2025
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Lazaro Kilahala, ametoa wito kwa Mameneja na Wahasibu wa mikoa yote kuhakikisha vituo vyao vinaongeza uwajibikaji na kujenga uwezo wa kujitegemea kiuchumi, badala ya kuendelea kuwa tegemezi kwa Serikali.
Akizungumza katika kikao kazi cha majadiliano ya utekelezaji wa mkakati wa mabadiliko ya TEMESA kilichofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya TEMESA, jijini Dodoma, Kilahala amesema taasisi hiyo ipo katika kipindi muhimu cha mabadiliko chanya, hivyo ni lazima kila mmoja atimize wajibu wake kikamilifu.
"Kama meneja wa mkoa unayeitambua thamani ya nafasi yako, ni wakati sasa uanze kuutazama mkoa wako kama familia yako ambayo ni lazima uiendeshe kwa ufanisi na kuihudumia kila siku. Tunataka kuona vituo vyetu vinaongeza mapato, vinatoa huduma kwa viwango na vinaepuka utegemezi usio wa lazima," amesema Kilahala.
Ameongeza kuwa ni jukumu la kila meneja na mhasibu kuhakikisha fedha zinatumika kwa makini, kwa kuzingatia vipaumbele vya maendeleo ya kituo, huku wakitumia ubunifu na mbinu za kitaalamu katika kuendesha shughuli zao.
Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa TEMESA, Bw. Moses Mabamba, amesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa watumishi katika hatua zote za upangaji wa bajeti za vituo.
Amesema kuwa mchakato wa bajeti haipaswi kuwa wa mtu mmoja au idara moja pekee, bali ni wajibu wa menejimenti kushirikisha watumishi wote ili kupata picha halisi ya mahitaji ya kila idara, hususan vitendea kazi vinavyohitajika kwa ajili ya utoaji huduma kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi, Mhandisi Hassan Karonda, ametilia mkazo dhana ya kujitegemea kuwa msingi muhimu wa heshima ya taasisi na kiongozi yeyote ndani ya TEMESA.
“Hakuna heshima kubwa kama kujitegemea. Ukitaka heshima kama taasisi au kiongozi, lazima ujenge uwezo wa kujiendesha bila kuwa tegemezi. Vituo vyetu vinapaswa kufikiria namna ya kuongeza mapato na kupunguza utegemezi kwa serikali,” alisema Mhandisi Karonda.
Alisisitiza kuwa kujitegemea kunaiwezesha taasisi kutoa maamuzi ya haraka, kuboresha huduma na kujiweka katika nafasi bora ya kuwahudumia wananchi. Aidha, alihimiza ubunifu na matumizi sahihi ya rasilimali kama njia ya kufikia lengo hilo.