​KILAHALA ATOA WITO KWA TAASISI ZA SERIKALI KUILIPA TEMESA MADENI YAKE

News Image

Posted On: February 03, 2023

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) ametoa wito kwa Taasisi za Umma na Serikali zinazodaiwa na Wakala huo baada ya kupatiwa huduma za matengenezo ya magari, mitambo, huduma za ufundi, umeme na elektroniki, kuilipa TEMESA madeni inayowadai ili Wakala huo uweze utekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Kilahala ametoa wito huo mapema leo, alipokuwa akizungumza katika kikao cha Wadau wanaopatiwa huduma na TEMESA Mkoa wa Dodoma, kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ulioko Makole mjini Dodoma ambapo kimehudhuriwa na maafisa mbalimbali wanaowakilisha Taasisi za Umma wakiwemo maafisa usafirishaji, maafisa kutoka Serikali kuu, Wizara mbalimbali, wawakilishi wa karakana teule zinazofanya kazi kwa pamoja na TEMESA pamoja na wazabuni wanaosambaza vipuri na vitendea kazi mbalimbali kwa Wakala huo.

Mtendaji Mkuu amesema, anafahamu changamoto ambazo wanakutana nazo kwenye Taasisi zao ikiwemo kutokutosha kwa mgawanyo wa fedha za maendeleo lakini akawataka kulipa uzito suala la kulipa madeno yao kwa TEMESA kwakuwa ili wao (Taasisi) waweze kufika kwa mwananchi kumpatia huduma wanahitaji kuwa na usafiri wa uhakika na ili wawe na usafiri wa uhakika, TEMESA inahitaji kuwa na uhakika wa kupata vipuri vya kuwatengenezea magari ya Taasisi zao kwahiyo kwa kutowalipa TEMESA kwa wakati kutasababisha ishindwe kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwani Wakala pia utakosa vipuri vya kuwatengenezea magari ya Taasisi zao na hivyo kurudisha nyuma maendeleo.

‘’Wito wangu mkubwa sana kwenye eneo la Matengenezo na Huduma za Ufundi, ni kwa wateja wetu, tunawaita washitiri, washitiri wetu tunawaomba chondechonde, suala la kutulipa mlitilie mkazo, kwasababu msipotulipa nyie huu mzunguko wa pembetatu tunaousema unakuwa hauna maana na unakufa, na ukifa sio faida kwenu, sio faida kwetu (Wakala), sio faida kwa wazabuni, lakini sio faida kwa nchi, kwahiyo tujitahidi sana kadiri ya uwezo wetu, najua changamoto ni nyingi lakini tulipe uzito unaostahili suala hili, tulitilie mkazo sana suala hili na tujitahidi kadiri ya uwezo wetu.’’ Amesema Mtendaji Mkuu na kuongeza kuwa TEMESA ipo kwa ajili ya kuhudumia wananchi na hivyo kama wakiamua kuzuia magari ambayo Taasisi zake hazilipi madeni yao maana yake watasababisha mwananchi akose huduma anayostahili kuipata na hivyo Wakala unaweka uzalendo mbele ili kuhakikisha mwananchi anapata huduma anayoistahili na hivyo Taasisi hizo zinapaswa kuweka uzalendo mbele kwa kulipa kwa wakati madeni yao.

Akizungumza kuhusu madeni ambayo Wakala unadaiwa na wazabuni ambao waliikopesha vipuri miaka ya nyuma, Kilahala amesema TEMESA haipuuzii na wala haijasahau kama inadaiwa na wazabuni hao, na ina wajibu wa kuwalipa. Mtendaji Mkuu amesema kuwa ipo timu ambayo imekwishaundwa kwa ajili ya kuyahakiki madeni hayo ikiwashirikisha wataalamu kutoka TEMESA, Wizara ya Ujenzi, Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali, wataaalamu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na wataalamu kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).

‘’Niwaombe tuwe wavumilivu na tuzidi kuamini kwamba hakuna mtu ambaye atadhulumiwa,mmemskia nyie wenyewe Mhe. Rais mara kwa mara anaweka wazi kwamba yeye hataki kuendesha Serikali ya dhulma, hataki kuona mtu anapoteza haki yake kwasababu amefanya kazi na Serikali, na sisi ni watekelezaji wa yale maagizo kwa hiyo msimamo na dhati ya Serikali ni kuhakikisha kwamba kila mwenye haki yake ataipata, kwahiyo niwatoe hofu’’ Alimaliza Mtendaji Mkuu.

Naye Meneja wa TEMESA Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Greyson Maleko, akizungumza katika kikao hicho, amewashukuru wadau wote waliohudhuria kikao hicho zikiwemo Taasisi ambazo hazikuvuka na madeni kwa mwaka uliopita. Mhandisi Maleko alimuongoza Mtendaji Mkuu kutoa tuzo ya kutambua mchango kwa Mashirika na Taasisi za Umma na Serikali kuu ambazo zimekuwa na mwendelezo wa kulipa madai wanayodaiwa na ofisi za Wakala huo kwa Mkoa wa Dodoma kwa wakati bila kuchelewa. Kilahala amezishukuru Taasisi hizo kwa kuendelea kulipa madeni yao kwa wakati na kuwaahidi kuwa Wakala utaendelea kuwapatia huduma iliyo bora wakati wote na kwa ufanisi mkubwa ili na wao waweze kutekeleza majukumu yao kwa wakati na kwa ufanisi.