KASEKENYA AWAKUMBUSHA WATUMISHI TEMESA KUTAMBUA DHAMANA WALIYOPEWA

News Image

Posted On: April 12, 2023

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Mhandisi Godfrey Kasekenya amewataka watumishi wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania kutambua dhamana waliyopewa na Serikali ni kubwa na hivyo wanapaswa kutambua umuhimu wa kuwepo kwa Taasisi hiyo na kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa ili kuleta tija kwa Serikali na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Kasekenya ameyasema hayo leo wakati alipohudhuria kikao cha Baraza la wafanyakazi wa Wakala huo kama mgeni rasmi, kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mjini Dodoma.

Kasekenya amesema dhamana waaliyopewa TEMESA si dhamana ndogo na haipaswi kupewa watu wengine ambao si Serikali, amewataka TEMESA kuhakikisha inakua Taasisi ambayo kila mtu akienda anasema kweli hii ni Taasisi ya Serikali.

‘’Dhamana ambayo mmepewa kwanza inahusisha Maisha ya Watanzania, lakini kikubwa kabisa inahusisha Maisha ya viongozi wetu wote, nyinyi ndio mnasimamia vivuko, lakini nyinyi ndio mnaosimamia matengenezo ya magari yote ya Serikali na viongozi kwa ujumla wake, lazima tujue dhamana ambayo tunatakiwa tuitekeleze.’’

Naibu Waziri pia ameitaka TEMESA kujiuliza kama wameundwa kama Taasisi kwa ajili tu ya kutoa huduma kwa Serikali au kujiendesha kibiashara.

‘’Nilikuwa nanong’ona na Mtendaji Mkuu, TEMESA ni Taasisi inayotoa huduma au ni Taasisi inayotakiwa kujiendesha kibiashara, Kimuundo wake ni Taasisi inayotakiwa kujiendesha kibiashara, je tunajiendesha kibiashara, je tuna ushindani ambao unatufanya tushindwe kujiendesha kibiashara, je hatuna wateja, kama ushindani nao ni mdogo nini zifanyike, pengine tunakosa ubinifu au tunafanya kazi kimazoea’’. Amesisitiza Mhe. Kasekekenya na kuongeza kuwa TEMESA inaweza kuingia ubia na makampuni makubwa ya kiJapan waweze kufungua viwanda vyao hapa nchi na hiyo itasaidia kampuni hizo kuuza vipuri halisi hapa nchini lakini pia kuongeza ajira kwa Watanzania na kuongeza kipato kwa Taifa.

Aidha, Mtendaji Mkuu wa Wakala huo, Lazaro N. Kilahala, akizungumza katika kikao hicho amesema Wakala unatarajia kuokoa zaidi ya shilingi Bilioni moja nukta mbili (1.2) kwa mwaka baada ya kuanza utaratibu wa kununua vilainishi moja kwa moja kutoka kwa watengenezaji wa vilainishi hivyo tofauti na hapo awali ambapo walikuwa wakinunua kutoka kwa wazabuni wa kati.

‘’Katika eneo la ununuzi wa vilainishi, utaratibu tuliojiwekea kama nilivoeleza hapo awali umetuelekeza kununua moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji kinyume na utaratibu wa awali ambapo tulikuwa tunanunua kwa wauzaji wa kati na fedha hizi tunazoziokoa zitaenda uboresha utedaji kazi wa karakana zetu.’’

Kilahala akizungumzia changamoto zinazoukabili Wakala huo amesema mojawapo ya changamoto kubwa inayoukabili Wakala ni ulipwaji wa madeni ambayo TEMESA inazidai Taasisi mbalimbali na Wizara hapa nchini, Kilahala amesema kuwa ulipwaji wa madeni hayo kutoka kwa washitiri umekuwa wa kusuasua na hivyo kusababisha Wakala kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

‘’Eneo lingine ni mrundikano wa madeni hasa kwenye kazi za karakana, ulipaji wa washitiri wetu bado ni wakusuasua lakini yapo mapendekezo ambayo tumeyaweka kwenye mkakati wa mabadiliko ya utendaji kazi wa TEMESA, nadhani tutakapofikia maamuzi basi tunaweza kuwa na jibu katika hili.’’ Amesema Kilahala na kuongeza kuwa bei za vipuri kuwa juu na udhibiti hafifu wa soko la vipuri ambao unasababisha uingiaji wa vipuri visivyo na ubora nalo pia ni changamoto kubwa ambayo Wakala unakabiliana nayo.

Mtendaji Mkuu pia amesema Wakala umeanza kutoa mafunzo kwa mafundi wa karakana zake ili kukabiliana na changamoto ya wataalamu na amesema tayari mafundi 85 wamepelekwa kwenye mafunzo na ameongeza kuwa zoezi hilo ni endelevu hivyo mafundi wote watapelekwa mafunzoni kwa makundi.

Kikao hicho cha Wafanyakazi kilimteua pia Katibu mpya wa Baraza hilo Bi. Cecilia A. Mugyabuso, Mhasibu kutoka karakana ya Mkoa wa Dodoma ambaye anachukua nafasi hiyo kutoka kwa Katibu wa Baraza aliyepita.