KASEKENYA ATOA WITO KWA WADAU WA TEMESA KUUNGA JUHUDI ZA MABADILIKO ILI ADHMA ILIYOPANGWA NA WAKALA IWEZE KUTIMIA
Posted On: March 24, 2025
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema kuwa Serikali imeridhia Wakala kutekeleza mkakati wa kuboresha utendaji kazi ambapo lengo kuu ni kuifufua TEMESA kutokana na malalamiko ya muda mrefu ya utendaji usiyoridhisha.
Kasekenya ameyasema hayo leo wakati akifungua kikao cha mkutano wa baraza la wafanyakazi wa TEMESA kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Morena mjini Morogoro ambapo amewaomba na kutoa wito kwa wadau wote wanaohudumiwa na TEMESA kuunga mkono mabadiliko haya ili adhma hiyo muhimu kwa mustakabali wa Taifa iweze kutimia.
Naibu Waziri amesema kuwa watumishi wanayo kazi ya kuuelewa na kutafsiri vyema mkakati wa mabadiliko haya na kuwasiliana na wanaowaongoza kwa lugha nyepesi inayoweza kueleweka ili TEMESA iweze kufikia malengo iliyojiwekea .
“mabadiliko haya ni zaidi ya kubadilisha mifumo ya utendaji kazi, mabadiliko haya yanaanza na nyie watumishi wa TEMESA, mifumo hii inasimamiwa na watu ambo ndo nyie, Ninyi ndio ‘’Moyo’’ wa mabadiliko haya. Hivyo, mkiwa ni Viongozi na wengine mkiwa wawikilishi wa watumishi mnayo kazi kubwa ya kufanya katika safari hii ya mabadiliko” alisisitiza.
Aidha Naibu Waziri ameipongeza Menejimenti ya Wakala kwa kuanza kutekeleza maelekezo ya Serikali, husani utaratibu wa malipo kabla (pre-paid) na matumizi ya mfumo wa TEHAMA katika kazi za matengenezo.
Akitoa salamu kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mkurugenzi wa Rasilimali na Utawala wa Wizara ya Ujenzi Bwa.Mrisho Mrisho amesisitiza watumishi wote kushiriki moja kwa moja juhudi za serikali za maboresho ya Wakala kupitia mkakati wa utendaji kazi wa TEMESA.
“Mkakati huu ni wetu sote wizara na wakala hivyo tushirikiane kwa pamoja kutekeleza mkakati huu kwa manufaa mazima ya TEMESA, wizara na tutakao wahudumia” alisisitiza.
Awali Mwenyekiti wa baraza na Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Lazaro Kilahala ameishukuru Serikali na kusema kuwa Wakala umeanza ukurasa mpya wa kuboresha utendaji kazi wake hivyo amewataka watumishi wote wa Wakala kushikamana na kuwa na uelewa wa pamoja, kujituma na kufanya kazi kwa weledi na uadilifu wa hali ya juu.
“Nichukue fursa hii kuishukuru Serikali kwa kuridhia na kuelekeza Wakala kuanza kutekeleza Mkakati wa kuboresha utendaji kazi wake. Uamuzi huu ni hatua muhimu sana katika kuuwezesha Wakala kufikia maono yake na uamuzi huu umekuwa faraja kubwa kwa Uongozi na Watumishi wa Wakala, Niahidi kuwa tutakeleza maelekezo hayo kwa nguvu, maarifa na jitihada zetu zote” Alisema Kilahala.