KARONDA AWATAKA WAZABUNI KUUZA VIPURI VYENYE UBORA ILI KUIMARISHA HUDUMA ZA TEMESA

News Image

Posted On: June 03, 2025

Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi TEMESA, Mhandisi Hassan Karonda, amewataka wazabuni kuhakikisha wanatoa vipuri na vilainishi vyenye ubora unaokubalika ili mchakato wa mabadiliko ndani ya TEMESA uwe na mafanikio.

Akizungumza katika kikao cha wazabuni wanaoihudumia TEMESA Mkoani Dar es salaam, Mhandisi Karonda amesema kuwa mabadiliko yanayoendelea yanapaswa yaendane na ubora wa vifaa ili TEMESA iweze kutoa huduma bora kwa wateja wake.

"Ili utoe huduma nzuri basi lazima uuze kitu kizuri na chenye ubora stahiki hivyo nawaomba msiuze vifaa visivyo na ubora, nyinyi mkifanya vifaa vyenu kuwa bora TEMESA itakuwa bora zaidi” alisema Mhandisi Karonda

Mhandisi Karonda alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeridhia kuiboresha TEMESA kwa kufanya mabadiliko ya malipo kabla ya huduma, hivyo, ubora wa vifaa unaotolewa na wazabuni bado ni eneo nyeti linalohitaji usimamizi na uwajibikaji wa pamoja ili huduma zinazotolewa ziwe na viwango vya kitaalamu vinavyokubalika.

Aidha, Mhandisi Karonda alisisitiza wazabuni kuwa sehemu ya mabadiliko chanya yanayoendelea ndani ya TEMESA kwa kuzingatia masharti ya mikataba, kuchagua bidhaa zenye viwango vya juu na kuwa wabia wa kweli katika safari ya Taasisi hiyo kutoa huduma zenye ufanisi, uwazi na tija kwa taifa.