UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SERIKALI YA MWAKA WA FEDHA 2022/2023 KUPITIA WAKALA WA UFUNDI NA UMEME TANZANIA (TEMESA)

News Image

Posted On: February 10, 2023

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

MAFANIKIO YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA

UTEKELEZAJI WA BAJETI YA SERIKALI YA MWAKA WA FEDHA 2022/2023 KUPITIA WAKALA WA UFUNDI NA UMEME TANZANIA (TEMESA)

1.0UTANGULIZI

1.0.1Kuanzishwa kwa Wakala:

Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) ulianzishwa kwa Sheria ya Wakala wa Serikali Na. 30 ya mwaka 1997 na kutangazwa katika Gazeti la Serikali Na. 254 la tarehe 26 Agosti, 2005. Wakala ulizinduliwa rasmi tarehe 23 Juni, 2006.

TEMESA ilikasimishwa majukumu yote yaliyokuwa yanatekelezwa na Idara ya Ufundi na Umeme (E&M Division) iliyokuwa chini ya Wizara ya Miundombinu ili kuendelea kutoa Huduma Bora na Endelevu zenye kuwaridhisha Wateja.

1.0.2Majukumu ya Wakala:

Kwa mujibu wa Amri ya Uanzishwaji ya Wakala ya 2005 (Establishement Order, 2005) majukumu ya Wakala ni kama ifuatavyo;

i.Kufanya matengenezo ya magari, pikipiki na Mitambo ya Serikali katika karakana ambazo zipo kila Mkoa;

ii.Kufanya matengenezo na Usimikaji wa mifumo ya Umeme, Mabarafu, Viyoyozi na Elektroniki inayomilikiwa na Serikali;

iii.Uendeshaji na Usimamizi wa Vivuko vya Serikali;

iv.Kutoa ushauri wa kitaalam kwa Serikali na Umma kwa ujumla katika Nyanja za Uhandisi wa Mitambo, Umeme na Elekroniki; na

v.Kukodisha mitambo mbali mbali kama vile mitambo ya kuzalisha kokoto na mitambo ya kazi za barabara.

Majukumu haya yanatekelezwa upande wa Tanzania Bara pekee.

1.0.3Muundo wa Wakala:

Ili kutekeleza majukumu haya kwa ufanisi, Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) una Kurugenzi tatu (3) ambazo ni Kurugenzi ya Huduma Saidizi (Business Support Services Directorate); Kurugenzi ya Matengenezo na Huduma za Ufundi (Maintenance and Technical Services Directorate) na Kurugenzi ya Ujenzi na Uendeshaji wa Vivuko (Ferry Operations and Construction Directorate).

Wakala una Vitengo vitano (5) ambavyo ni Kitengo cha Usimamizi wa Ununuzi; Kitengo cha Huduma za Sheria; Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani; Kitengo cha TEHAMA na Takwimu; na Kitengo cha Masoko na Uhusiano.

Aidha, Wakala una Ofisi za Kanda mbili (2) zinazosimamia uendeshaji wa Vivuko ambazo ni Kanda ya Mashariki na Kanda ya Ziwa, Ofisi za Mikoa ishirini na sita (26) na Ofisi za Wilaya tatu (3) zinazosimamia Karakana za Matengenezo na huduma za Ufundi.

2BAJETI YA WAKALA KWA MWAKA 2022/23

Katika mwaka wa fedha 2022/23 Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi iliidhinisha bajeti yenye jumla ya Shilingi 21,277,194,259/= kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayosimamiwa na TEMESA na jumla ya Shilingi 7,893,863,700/= kwa ajili ya mishahara na stahiki za watumishi.

Miradi hii inajumuisha Ujenzi wa Vivuko vipya (TZS 4,572,117,000/=), Ukarabati wa Vivuko (TZS 5,858,229,472/=), Ujenzi wa Miundombinu ya Vivuko (TZS 3,309,506,708/=), Ujenzi wa Karakana mpya (TZS 2,513,080,000/=), Ukarabati wa Karakana (TZS 1,000,000,000/=), Ununuzi wa Vipuri na Vitendea kazi (TZS 1,554,296,000/=), Ununuzi wa mifumo ya TEHAMA (TZS 2,016,532,798/=), Usimamizi wa Miradi na Mafunzo (TZS 435,432,281/=).

Aidha, katika mwaka wa fedha 2022/23 Wakala ulijipangia kuzalisha jumla ya Shilingi 90,435,876,240/= kama mapato ghafi kupitia shughuli zake za Matengenezo na Ufundi, Usimamizi wa Vivuko, Ukodishaji wa Mitambo na Huduma za Ushauri.

3UTEKELEZAJI WA BAJETI YA WAKALA MWAKA 2022/23

Utekelezaji wa miradi ya maendeleo:

Wakala umesaini mikataba mitano (5) ya Ujenzi wa vivuko vipya vya Kisorya-Rugezi, Ijinga-Kahangala, Bwiro-Bukondo, Nyakarilo-Kome na Mafia-Nyamisati yenye thamani ya Shilingi Bilioni 33.2 ambapo hadi kufikia mwezi Januari 2023 jumla ya Shilingi Bilioni 10.3 zilikwishalipwa kama malipo ya awali na Ujenzi wa Vivuko hivi unaendelea. Aidha, Wakala unakamilisha taratibu za Ununuzi wa Kivuko cha Buyagu-Mbarika na ‘Sea Taxi’ mbili.

Wakala umesaini mikataba kumi na sita (16) ya Ukarabati wa Vivuko yenye thamani Shilingi Bilioni 23.3 ambapo hadi kufikia mwezi Januari 2023 jumla ya Shilingi Bilioni 7.96 zilikwishalipwa na kazi zinaendelea. Aidha, ukarabati wa vivuko sita (6) kati ya hivyo – MV. KAZI, MV. MUSOMA, MV. KILAMBO, MV. SABASABA, MV. TEMESA NA MV. TANGA umekamilika.

Wakala umesaini mikataba kumi na moja (11) ya Ujenzi na Ukarabati wa Maegesho na Miundombinu ya Vivuko yenye thamani ya Shilingi Bilioni 4.12 ambapo hadi kufikia mwezi Januari 2023 jumla ya Shilingi Bilioni 1.79 zilikwishalipwa na kazi zinaendelea.

Wakala umesaini mikataba mitano (5) ya Ukarabati wa Karakana na Mikataba miwili (2) ya Ujenzi wa Karakana Mpya za Mikoa ya Simiyu na Dodoma yenye thamani ya Shilingi Bilioni 7.44 ambapo hadi kufikia mwezi Januari 2023 jumla ya Shilingi Milioni 830.5 zilikwishalipwa. Aidha, Ujenzi wa Karakana ya Simiyu umekamilika na Wakala unaendelea na taratibu za Ununuzi ili kuanza Ujenzi wa Karakana za Geita na Njombe.

Wakala umesaini mikataba miwili (2) ya Ununuzi na Usimikaji wa Mifumo ya Kielektroniki yenye thamani ya Shilingi Milioni 910.8 ambapo hadi kufikia mwezi Januari 2023 jumla ya Shilingi Milioni 435.8 zimekwishalipwa. Aidha, usimikaji wa mfumo wa Ncard katika kituo cha Magogoni-Kigamboni umekamilika.

Kwa ujumla, hadi kufikia mwezi Januari 2023 Wakala umesaini mikataba ya utekelezaji wa miradi yenye thamani ya Shilingi Bilioni 71.96 ambapo jumla ya Shilingi Bilioni 23.65 zimekwishalipwa ambapo kati ya fedha hizo jumla ya Shilingi Bilioni 15.625 zimetolewa na Serikali ndani ya mwaka huu wa fedha. Kiasi kilichobaki kitaendelea kulipwa kadiri utekelezaji unavyofanyika na hati za madai kuwasilishwa.

Utendaji wa Wakala katika mwaka wa fedha 2022/23:

Hadi kufikia Disemba 31, 2022 Wakala ulifanikiwa kuzalisha mapato ghafi ya jumla ya Shilingi Bilioni 31.53 sawa na asilimia 35 ya lengo la mwaka la kuzalisha Shilingi Bilioni 90.43. Utendaji wa Wakala uliathiriwa na uchakavu wa vivuko pamoja na mabadiliko ya kiutendaji yaliyotekelezwa na Wakala katika nusu ya kwanza ya mwaka. Hata hivyo utendaji unatarajiwa kuimarika kadiri mabadiliko yanavyozoeleka na ukarabati wa vivuko unavyokamilika.

Kazi zinazoendelea kutekelezwa na Wakala katika mwaka wa fedha 2022/23 zimeainishwa hapa chini: -

Kusimamia uendeshaji na matengenezo ya vivuko.

Matengenezo ya magari, pikipiki na mitambo ya Serikali kupitia mtandao wa Karakana 27 kote nchini, Tanzania Bara.

Usimikaji wa mifumo ya umeme na elektroniki katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Simiyu

Usimikaji wa mifumo ya Umeme na elektroniki katika Jengo la Mama na Mtoto, Hospitali ya Mawenzi Kilimanjaro.

Usimikaji wa mifumo ya Umeme na elektroniki katika majengo ya Ofisi za Halmashauri ya Miji ya Kahama na Bariadi

Usimikaji wa mifumo ya umeme na elektroniki katika kiwanda kipya cha Bohari ya Madawa (MSD) kilichopo Idofi Makambako Njombe

Usimikaji wa mifumo ya umeme na elektroniki katika majengo ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora yaliyopo Mji wa Serikali (Magufuli City) Mtumba mjini Dodoma.

Usimikaji wa mfumo wa taa na kamera za usalama barabarani katika mji wa Serikali (Magufuli City) Mtumba mjini Dodoma.

Usimikaji wa taa za barabarani katika Halmashauri ya Manispaa ya Mji Singida eneo la Kintinku na eneo la Malendi.

Usimikaji wa taa za barabarani Wilayani Ruangwa mkoni Lindi.

Matengenezo kinga ya taa za barabarani kote nchini.

Kutoa ushauri wa kitaalamu katika Ujenzi wa majengo mbalimbali katika mji wa Serikali (Magufuli City) Mtumba mjini Dodoma.

4CHANGAMOTO

Changamoto kubwa zinazoukabili Wakala kwa sasa ni nauli za vivuko zilizopitwa na wakati, zisizoendana na bei ya soko wala Gharama halisi za uendeshaji wa vivuko pamoja na ulipaji usioridhisha wa wateja wanaohudumiwa na Wakala hasa katika matengenezo ya magari, pikipiki na mitambo.

5HITIMISHO

Kipekee kabisa Wakala unaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi chini ya Mhe. Waziri Prof. Makame M. Mbarawa na Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi Mhe. Balozi Mha. Aisha S. Amour kwa kufanikisha upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa miradi iliyotajwa hapo juu, muongozo wa kisera, usimamizi na maelekezo ya mara kwa mara yanayowezesha Wakala kutekeleza majukumu yake kwa mafanikio.

Aidha, Wakala unawashukuru viongozi mbalimbali wa Serikali na Taasisi zake kama vile Makatibu Wakuu, Wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga Wafawidhi wa Hospitali na wengineo wote kwa kuendelea kutuamini na kutupatia kazi mbalimbali.

Wakala tunaendelea kuboresha huduma zetu na tunawaahidi kuongeza ufanisi na tija ili kufikia malengo na matarajio yao na wananchi kwa ujumla.

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA

KAZI IENDELEE