SERIKALI KUJENGA SEA TAX MBILI MAGOGONI FERI
Posted On: January 20, 2023
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeahidi kujenga vivuko vipya vidogo viwili vinavyoenda haraka (Sea Tax) vitakavyokuwa vinatoa huduma kwa wakazi wa Magogoni na Kigamboni jijini Dar es Salaam kutokana na uhitaji mkubwa wa usafiri unaowakabili wakazi wa maeneo hayo.
Hayo yamebainishwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro Kilahala wakati akizungumza na waaandishi wa Habari makao makuu ya Wakala huo mjini Dodoma. Kilahala amesema Mji wa Kigamboni na viunga vyake unakua kwa kiasi kikubwa sana hivyo kutokana na kuongezeka kwa wakazi maeneo hayo, Serikali imeamua kuwa itajenga vivuko hivyo vipya vya Kwenda haraka vitakavyokuwa vinatoa huduma kati ya Magogoni na Kigamboni ili kupunguza kero ya usafiri kutokana na uwepo wa abiria wengi wanaotumia huduma za kivuko.
‘’Sasa hivi tunakamilisha hatua za manunuzi, Serikali iliamua kwamba tununue vivuko vidogo viwili aina ya (Sea Tax) na hii ni baada ya kuona ufanisi wa vile vivuko viwili vya Azam vinavyofanya kazi pale kwa sasa ambavyo vinavusha abiria kwa wakati mfupi zaidi, kama utakumbuka miongoni mwa vitu ambavyo ni kero kubwa kwa wananchi wetu pale ni muda wanaopoteza wakati wanasubiri kupata huduma na hivyo ikaonekana vivuko vidogo ndiyo itakua tija zaidi kwa ajili ya kuwavusha watu kwa uharaka zaidi, kwahiyo taratibu za manunuzi zinakamilishwa sasa hivi nadhani wako kwenye hatua za tathmini na wakishamaliza tutasaini mikataba kwa ajili ya kukamilisha ununuzi huo.’’ Alisema Kilahala.
Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba baada ya bajeti kuanza ya mwaka 2022/2023 zinatengwa fedha kwa ajili ya kuanza mara moja ujenzi wa vivuko vipya na kwa pamoja vivuko hivyo vikishirikiana na vingine vitatu vinavyotoa huduma katika eneo hilo kikiwemo kivuko cha MV. KAZI, MV. MAGOGONI na MV. KIGAMBONI, tatizo la usafiri katika maeneo kati ya Magogoni na Kigamboni litapungua kwa kiasi kikubwa.