SERIKALI KUJENGA KARAKANA MPYA TEMESA

News Image

Posted On: July 31, 2023

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) imetenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa karakana mpya nne zitakazoanzwa kujengwa katika mwaka huu wa fedha wa 2023/2024.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi wa Wakala huo Mhandisi Hassan Karonda wakati alipofanya mahojiano maalumu na maofisa wa Kitengo cha Masoko na Uhusiano wa Wakala huo mjini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita. Mhandisi Karonda amezitaja karakana mpya zitakazojengwa kuwa ni za Mikoa ya Geita, Songwe, Njombe na Katavi huku karakana ya Mkoa wa Simiyu ikijengwa kwa awamu ya pili baada ya ujenzi wa awamu ya kwanza kuwa tayari umekamilika.

Mhandisi Karonda amebainisha kuwa Serikali imekuwa ikiendelea kutoa fedha kila mwaka kwa ajili ya ujenzi wa karakana mpya, ukarabati wa karakana zilizochakaa pamoja na ununuzi wa vitendea kazi vipya vya karakana kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa Wakala.

‘’Karakana hizo mpya zitajengwa katika Mikoa ya Njombe, Songwe na Katavi,vilevile tutajenga karakana mpya Mkoa wa Geita ambayo kwa sasa hivi iko kwenye hatua ya kubuni (designing), tumeshapata Mhandisi Mshauri ambaye amekwishafanya ubunifu kwahiyo kwa sasa tuko kwenye hatua ya kutangaza ili kumpata mkandarasi kazi hiyo ianze kwasababu fedha zipo, Mkoani Simiyu, karakana tayari ilikwishajengwa awamu ya kwanza (phase one) na tayari imekwishakamilika, kwa sasa tunataka kuanza ujenzi kwa awamu ya pili (phase two) tayari mkandarasi amekwishapatikana hivyo awamu ya pili ya ujenzi huo inaanza muda si mrefu.’’ Amesema Mhandisi Karonda.

Mhandisi Karonda ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Ujenzi kwa kuendelea kuboresha karakana za Wakala huo kwa kuzifanyia maboresho makubwa ikiwemo kukarabati karakana zilizochakaa pamoja na kununua vitendea kazi vipya kwa kila karakana Nchini ambao amesema utaratibu huo utaendelea kuboresha utoaji huduma na kuchochea ari katika utendaji kazi wa Karakana.