TAASISI ZA UMMA MKOANI NJOMBE ZAAGIZWA KULIPA SHILINGI MILIONI 800 INAZODAIWA NA TEMESA

News Image

Posted On: January 25, 2024

Kaimu Katibu Tawala (RAS) Mkoa wa Njombe Bwana Ayoub Mndeme ametoa rai kwa Taasisi zote za Serikali Mkoani humo kuhakikisha zinalipa madeni ambayo zinadaiwa na ofisi ya Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Mkoa wa Njombe ili kuuwezesha Wakala huo kuweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kutoa huduma bora kwa Taasisi za Serikali Mkoani humo.

Bwana Mndeme ametoa rai hiyo Tarehe 24 Januari 2024 wakati alipokuwa akizungumza katika Kikao cha Wadau wanaotumia huduma za Wakala huo kilichofanyika katika Hoteli ya Agreement iliyoko Mjimwema Mkoani Njombe huku akimuahidi Mtendaji Mkuu kwamba endapo kutakuwa na changamoto zinazoendelea kujitokeza kuhusiana na ulipaji wa madeni hayo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Njombe itakuwa tayari kuongeza nguvu kwa kushirikiana bega kwa bega na TEMESA kuhakikisha madeni hayo yanalipwa kwa wakati na kumalizika.

‘’Tumeelezwa changamoto nyingine ni madeni, tunafahamu sisi tulikuwa na changamoto zetu lakini kuna nyingine zina tuhusu sisi, kwahiyo nitoe rai kwa Taasisi zote ambazo zinadaiwa madeni kwa ujumla wake kwa mfano Mkoa wa Njombe nilisikia inatajwa hapa, tunadaiwa shilingi Milioni 800, sasa hizi ni pesa nyingi sana ambazo zinaweza kutusaidia kuiwezesha TEMESA ikaweza kutimiza ile mikataba ambayo imekuwa ikiingia labda pengine na wazabuni na kampuni mbalimbali ambazo zinatoa huduma ambazo zinakuja kutunufaisha.’’ Alisema Bwana Mndeme.

Aidha, Kaimu Katibu Tawala Mndeme pia ameongeza kuwa Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya kununua vitendea kazi kwa TEMESA ikiwemo karakana inayotembea (Mobile Workshop), na kusema kuwa hiyo ni hatua kubwa kufanywa na akaupongeza Wakala huku akiishukuru Serikali kwa kutoa fedha za ununuzi wa vitendea kazi hivyo pamoja na kutoa ajira kwa mafundi pamoja na kuwapeleka mafunzoni mara kwa mara ili kuwaongezea ujuzi na taaluma kwakua hatua hiyo itasababisha huduma kuboreshwa kwa kiasi kikubwa na Mkoa wa Njombe kuweza kunufaika na upatikanaji wa huduma bora na kuongeza ufanisi kwa watumishi wa TEMESA.

‘’Nataka kuendelea kusisitiza kwamba sisi tuna matumaini makubwa sasa na TEMESA ambayo naamini kabisa inakwenda kubadilika, kutoa huduma bora, malalamiko kwakweli yalikuwa ni mengi lakini bahati nzuri mmekaa na kujitathmini na sisi tunayo imani kubwa kwasababu ni Taasisi ya Serikali kwamba kile ambacho mmekuja kukisema hapa ndicho kinakwenda kutekelezwa.’’ Alisisitiza Bwana Mndeme.

Naye Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi kutoka Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Mhandisi Hassan Karonda ambaye alimuwakilisha Mtendaji Mkuu wa Wakala huo, akizungumza katika kikao hicho amesema, mpaka sasa, kwa Nchi nzima TEMESA inazidai Taaasisi za Umma zaidi ya shilingi Bilioni 50 huku akisisitiza kwamba fedha hizo ni nyingi sana na kwa kiasi kikubwa zinaathiri kwa namna moja ama nyingine utendaji wa kazi wa Wakala.

‘’Kwahiyo tufanye tunavyofanya lakini kuhakikisha kwamba tunapata huduma nzuri, ndugu zangu, watumishi wenzangu, tuhakikishe tunaiwezesha TEMESA kwa kulipa kwa wakati ili tuweze kuhudumia na mipango hii tunayoizungumza yote iweze kwenda kutimia, kwasababu kama hatutoweza kulipa kwa wakati, hii mipango inaweza ikawa tofauti kwasababu hatuna sehemu ambayo tunapata vipuri bure, vipuri hivi tunanunua na wazabuni wanahitaji kulipwa.’’Alimaliza Mhandisi Karonda.

Vilevile, miongoni mwa waliohudhuria kikao hicho, alikuwa ni Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi CCM) MNEC Mkoa wa Njombe Bwana Daniel Okoka ambaye akizungumza mara baada ya kupewa nafasi katika kikao hicho, amesema hatua ya kujitathmini kwa walio wengi ni hatua ngumu na watu wengi hata mashirika hayapendi kuifanya kwa kuhisi inaonyesha mapungufu yao, lakini TEMESA kwa kulitambua hilo kwa makusudi kabisa imeamua kuwa na mikutano ya namna hiyo ili kujitathmini ilipotoka, ilipo na inakokwenda.

‘’Kwakweli tunaona matumaini kwasababu mimi binafsi nimekua mdau wa TEMESA kwa maana ya Mwenyeiti wa Halmashauri, tulikuwa na migogoro mingi sana ya namna TEMESA inavyofanya kazi na wakati fulani ikafikia mahali Taasisi zetu zinaikimbia TEMESA, sasa hili jambo kimsingi halikuwa linaleta taswira nzuri kwa maana Taasisi ya Serikali inakimbiwa na wanaotakiwa kuitumia, ilikuwa ni tatizo.’’ Alisema Bwana Okoka na kuongeza kuwa wana Imani mapinduzi yanayofanywa na Wakala huo yatakwenda kuleta mageuzi makubwa ndani ya TEMESA.

Bwana Okoka pia ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo ameendelea kujenga uwezo wa Taasisi mbalimbali ikiwemo TEMESA na kuongeza kuwa maono hayo, Wakala unapaswa kuyabeba ili mwisho wa siku waweze kufikia kwenye maono ya Mheshimiwa Rais.

Awali, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi kutoka TEMESA Bi. Josephine Matiro akizungumza katika kikao hicho amesema, lengo la vikao hivyo ni kuuleta Wakala huo karibu na wadau wake, kupokea maoni, ushauri pamoja na kutoa mrejesho wa yale ambayo Wakala huo umeahidi kuyatekeleza ili kuboresha huduma kwa wateja wake hivyo kama Wakala, wamekaa wakajitathmini na kujikosoa na kuona ipo sababu ya kupita Mikoani na kuweza kuzungumza na wadau kwasababu Wakala huo una ofisi katika Mikoa yote ishirini na sita Nchi nzima. ‘’Ipo sababu ya kupita na kuongea na wadau wetu tujue changamoto zetu ni zipi, matatizo yanayotukumba ni yapi, na hii yote tunafanya ili tuweze kufanya marekebisho.’’ Alisema Bi. Josephine.

Mkoa wa Njombe sasa unakuwa ni wa Ishirini na moja tokea Wakala huo uanze utaratibu wa kukutana na kufanya vikao na wadau wake na kikao kinachofata kinatarajiwa kufanyika Mkoani Songwe siku ya Ijumaa yaTarehe 26 Januari 2024.