SERIKALI KATIKA KASI YA UJENZI, UKARABATI WA VIVUKO KANDA YA ZIWA
Posted On: December 19, 2023
Muda si mrefu Mikoa ya Kanda ya Ziwa itaondokana na adha ya usafiri kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika ujenzi wa vivuko vipya na kukarabati vya zamani. Ujenzi na ukarabati wa vivuko hivyo ni mradi unaotekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA). Mtendaji Mkuu wa TEMESA Lazaro Kilahala hivi karibuni alisema adha ya usafiri kwa ukanda huo itakwisha. Alikuwa jijini Mwanza katika ziara ya ukaguzi wa vivuko vinavyojengwa na kukarabatiwa na kampuni ya Songoro Marine.
Alisema katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali inamalizia ukarabati wa vivuko 11 vinavyogharimu shilingi bilioni 24.8 ambapo kati ya hivyo, 10 tayari vimekamilika na vimeanza kutoa huduma ya kusafirisha abiria. Kilahala alisema vivuko viwili bado vinaendelea kufanyiwa ukarabati. Alisema kwenye ujenzi na ukarabati huo, Serikali imewekeza shilingi bilioni 70.
''Huu ni uwekezaji mkubwa, unaonyesha kwa vitendo nia ya dhati ya Serikali yetu kuondoa changamoto za usafiri zinazowakabili wananchi hasa kwenye maeneo ya Visiwani.'' Alisema. Alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika eneo hilo kuhakikisha maisha ya Mtanzania yanaimarika.
Alisema TEMESA pia ina jukumu la matengenezo ya magari na ili kuliboresha eneo hilo Serikali imeiwezesha TEMESA kufanya ukarabati wa karakana za Mikoa ya Mwanza, Mara, Tabora na Kigoma ikiwa ni sehemu ya uwekezaji unaoendelea kwenye Mikoa hiyo.
''Serikali inataka kuona kila nyanja ya huduma inayotolewa na TEMESA inaimarika ili Mtanzania ahudumiwe kwa ubora na ufanisi zaidi.'' Alisema.
Kilahala alimhakikishia Rais Samia na Serikali kwamba TEMESA inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kazi waliyotumwa wataifanya kwa weledi. ''Tutaifanya kwa uhakika na tutahakikisha malengo tuliyopewa kuyatimiza yanatimia kwa wakati.'' Alisema.
Kilahala anasema ukarabati wa vivuko uko chini ya kampuni ya wazawa ya ujenzi wa meli na vivuko ya Songoro wanaofanya kazi hiyo ya ujenzi wa vivuko kwa weledi na uaminifu. Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Songoro Marine, Major Songoro alisema hivi karibuni kampuni yake imekamilisha ukarabati wa vivuko na tayari vimeshaanza kutoa huduma ya usafiri kwa wananchi.
Alivitaja vivuko hivyo kuwa ni MV. MARA ambacho kimekabidhiwa Oktoba 15, 2023, MV. MISUNGWI, MV. UJENZI ambacho kilifanyiwa ukarabati, MV. MUSOMA, vyote hivyo vimekamilika na vinatoa huduma kwa wananchi.
Songoro anasema anaendelea na ujenzi wa vivuko vitatu ambavyo kwa sasa viko kwenye hatua za ukarabati. Alitolea mfano kivuko cha MV. NYERERE ambacho kinafanyiwa marekebisho na ukarabati mkubwa na kimefikia asilimia 80.5%, kinatarajiwa kukamilika Januari 31, 2024. ''Tuna MV. KILOMBERO kiko katika asilimia 89%, MV.RUVUVU kiko asilimia 90% na sisi Songoro Marine tunaendelea kushirikiana na Serikali katika ujenzi wa vivuko vipya na vinavyofanyiwa ukarabati.'' Alisema Songoro.
Songor anasema kampuni yake imepata manufaa makubwa kutekeleza ukarabati na ujenzi wa miradi ya vivuko hivyo kwa Kanda ya Ziwa na wakazi wa Kanda hiyo hasa vijana wamenufaika kupata ujuzi.''Kampuni yetu inashirikiana na kampuni kubwa za nje zinazotupa Teknolojia kubwa ikiwemo ya kufanya ubunifu kwenye ukarabati na ujenzi wa vivuko.'' Alisema.
Alisema Teknolojia hiyo inayochumwa na Watanzania kutoka kwenye kampuni yake na zile za nje ina manufaa makubwa ya kiuchumi hasa kutoa ajira. '' Mzunguko mkubwa wa fedha wakati wa utekelezaji wa miradi hii unabaki hapa Nchini.'' Anasema Songoro. Anasema kampuni yake inazalisha ajira hadi nje ya Nchi kupitia Teknolojia ya ujenzi wa vivuko.
''Leo Songoro ina miradi mingi ya ujenzi wa vivuko Uganda, lakini bila kupata dhamana ya Serikali maana yake tusingepata kazi hiyo,'' anasema. Anasema vivuko hivyo vya Uganda vinajengwa na wataalamu zaidi ya watu 25 kutoka Songoro Marine ambao wako Nchini humo. '' Tunaishukuru Serikali na naiomba iendelelee kuziwezesha kampuni za ndani zikuwe na kuchochea ukuaji wa uchumi.'' Anasema.
Kaimu Meneja wa TEMESA Kanda ya Ziwa na Magharibi Mhandisi Vitalis Bilauri aliwahakikishia wakazi wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa kuwa vivuko hivyo vinajengwa na kukarabatiwa kwa ubora na ufanisi unaotakiwa kwa mujibu wa viwango vya Kimataifa. Anasema jukumu lake kubwa ni kusimamia ubora wa ujenzi wa vivuko vinavyojengwa na vile vinavyofanyiwa ukarabati na kwenye kusimamia ubora, kutekeleza ni kwa hatua.
Bilauri anasema katika kila hatua ya ujenzi wa vivuko, wataalamu wa TEMESA wanakuwepo kuhakikisha aina za vifaa na ujuzi unaotumika kwa madai kila aina ya kivuko ina vigezo vyake vya namna kinavyojengwa au kukarabatiwa.
''Lazima kiwe na uwezo fulani, kubeba kiasi gani cha mzigo na kinatakiwa kijengwe kwa utaratibu upi ambao utakifanya kuwa salama kitakapokuwa kinahudumia wananchi.'' Anasema.
Anasema yeye msimamizi kwa kushirikiana na wataalamu wengine anahakikisha kila hatua ya ujenzi au ukarabati unafanywa kwa ubora unaotakiwa. ''Tunahakikisha vifaa vya kutengeneza vivuko vinapowasili lazima tuhakikishe vipimo vinavyotumika vimezingatiwa.'' Alisema
Anasema hata kwa vinavyotoka nje ya Nchi zikiwemo mashine za aina mbalimbali za ijnini vinapowasili Nchini hukaguliwa ikiwemo kuangalia serial namba na mzalishaji wake (manufacturer) ili wajiridhishe ni yeye aliyetengeneza au kuzalisha kifaa husika. Anasema lengo ni kuhakikisha ubora unaotakiwa wa kiwango cha juu.
Wananchi wamezungumza akiwemo mkazi wa Misungwi Ramadhan John anamshukuru Raisi Samia kwa kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa miradi hiyo ya vivuko ambayo itakapokamilika itachochea ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya usafirishaji abiria, bidhaa na mizigo.
Imeandaliwa na Nashon Kennedy- Habari Leo Mwanza